Wakazi
wa jiji la Dar es Salaam, wameambiwa wachukue tahadhari na umakini
wakati wa kununua samaki nyakati za jioni, kutokana na madai kuwa baadhi
ya wachuuzi huvua kwa kutumia mabomu.
Tahadhari
hiyo imekuja baada ya kufanya uchunguzi wa muda mrefu, ambapo imegundua
samaki hao wanauzwa nyakati hizo kukwepa kugundulika.
Imefahamika
licha ya Serikali kuwa na kampeni ya kusaka watu wanaojihusisha na
uvuvi huo, bado hali imekuwa mbaya katika maeneo ya pwani ya bahari ya
Hindi.
Maeneo
yanayotajwa kukithiri kwa uvuvi wa mabomu ni Pwani ya Bagamoyo, Kawe
katika Manispaa ya Kinondoni na Buyuni eneo la Kigamboni, Manispaa ya
Temeke.
Baadhi ya
wavuvi waliofanikiwa kuzungumza na gazeti hili kwa masharti ya
kutotajwa majina yao kwa usalama, walisema watu wanaojihusisha na uvuvi
haramu wanatumia mbinu nyingi za kuingiza samaki sokoni.
Walisema watu
wengi kutokana na kuanza kuwabaini samaki wa aina hiyo, wavuvi
wanawauza kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu nyakati za jioni bila ya
kugundulika kwa urahisi.NA NIPASHE Jumapili
MBINU CHAFU
Mmoja wa
wavuvi hao, alisema njia nyingine iliyobuniwa ni kuwaweka kwenye
majokofu ili kuwafanya wawe wagumu kama wanavyokuwa samaki waliovuliwa
kihalali.
"Samaki
wa mabomu anakuwa laini kutokana na kuvunjwavunjwa na mlipuko, pia macho
yao yanaonekana mekundu kutokana na kuvilia damu", alisema na kuongeza
"Samaki wadogo wanauzwa kwa wakaanga samaki pale pale ufukweni."
Alisema, samaki wakubwa wanahifadhiwa kwenye jokofu kwa muda wa siku moja ili kuwagandisha na barafu.
"Ugumu wa barafu inasababisha kutopindika kirahisi, ni vigumu kumgundua kama amevuliwa kwa bomu," aliongeza kusema.
SOKO LA FERI
Katibu
Mkuu wa Soko la Kimataifa la samaki la Feri, Mbaraki Kilima,
akizungumzia suala hilo, alisema kwamba wamefanikiwa kudhibiti samaki
hao wasiingie kwenye mzunguko wa ndani ya soko hilo.
Hata
hivyo, alikiri kuna kipindi wanaingizwa kinyemela, lakini wengi wao
wanauzwa nje ya soko hasa maeneo ya kivuko cha Kigamboni.
"Ni kazi
ngumu kuwakabili wahusika kwa sababu wana vitisho, kilichobaki tunakuwa
makini samaki kuingia hapa kwetu pekee," anasema Kilima.
NI VIGUMU KUWAKAMATA
Baadhi ya wavuvi hao walisema ni vigumu kukamatwa kutokana na kuwa na mtandao mkubwa.
Walisema endapo kunatokea zoezi la kuwakamata, wanapata taarifa mapema, hivyo ni rahisi kwao kukimbia.
"Kuna
watu wanashirikiana nao sehemu mbalimbali, viongozi hata polisi, hata
sisi inatuwia vigumu kuwataja kwani tunaweza kuhatarisha maisha yetu,",
alisema mmoja wao.
AFISA UVUVI TEMEKE AZUNGUMZA
Afisa
Uvuvi wa Manispaa ya Temeke, Teddy Chuwa aliakiri kuwepo kwa hali hiyo,
ambapo alitoa takwimu ya watu zaidi ya 50 wamekamatwa na kupelekwa
Mahakamani.
Alisema wamekuwa na operesheni maalum za kuwakamata watu hao na kupelekea kupungua kwa matukio ya aina hayo kwa asilimia 70.
Chuwa
alifafanua kwamba kuna madhara ya kula samaki waliovuliwa kwa mabomu
japo hayajitokezi kwa haraka, hivyo alionya watu kutowanunua.
Afisa
huyo, alisema katika mazingira ya bahari, mabomu hayo yanaharibu
matumbawe ambayo ni mazalia ya samaki pamoja na kuharibu ikolojia ya
viumbe wanaoishi majini.
TFDA WAZUNGUMZA
Afisa
Uhusiano wa Mamlaka ya udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) Gaudensia
Simwanza, akizungumzia suala hilo alisema, kwamba bado hajapata taarifa
kuingia kwa samaki hao sokoni.
"Sisi
tunafanya kazi ya kuangalia samaki wanaoingia sokoni, lakini sijapata
taarifa yoyote kama kuna wa aina hiyo, ngoja niwasiliane na idara ya
chakula halafu nitatoa taarifa," alisema Simwanza.
Hata
hivyo, alisema kuwa udhibiti wa samaki hao unafanywa na idara ya uvuvi
kwa Halmashauri za jijini Dar es Salaam, endapo zoezi hilo likiendeshwa
kwa umakini samaki hao siyo rahisi kuingia sokoni na kuuzwa kiholela.
0 comments:
Post a Comment