Shekhe Ponda Issa Ponda akianza safari yake ya kuelekea Segerea ndani ya gari la Magereza jana. |
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu, Shekhe Issa Ponda, ameruhusiwa kutoka hospitalini katika
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI),
alikokuwa amelazwa na kupelekwa rumande katika gereza la Segerea.
Meneja Uhusiano wa MOI, Jumaa Almasi, alithibitisha jana Shekhe Ponda kuruhusiwa na kuongeza kuwa hatua hiyo ilitokana na madaktari kujiridhisha kuwa hali yake ni nzuri.
“Ni utaratibu wa kawaida kwa mgonjwa, hali yake ikionekana kwa kiasi fulani kuwa nzuri, hospitali humruhusu kurudi nyumbani wakati akiendelea kupata nafuu, ndivyo ilivyokuwa kwa Shekhe Ponda,” alisema Almas.
Alisema Shekhe Ponda alipewa ruhusa hiyo saa tano kasorobo asubuhi na baada ya hapo taratibu zingine za kuondoka kwake zilibaki kwa vyombo vya sheria vilivyokuwa na dhamana naye.
Alirejeshwa rumande ambako alitolewa Mei 10 baada ya kukaa kwa miezi saba, akishitakiwa kwa kesi ya jinai.
Katika kesi hiyo, Ponda alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi 12 kwa masharti ya kutofanya kosa katika kipindi hicho. Alipewa hukumu hiyo kwa vile hakuwa na kumbukumbu za kutenda makosa ya jinai na kwa vile alishakaa rumande kwa zaidi ya miezi saba.
Kabla ya kuchukuliwa jana hospitalini hapo, magari ya Polisi yakiwa na askari wa kuzuia fujo yalifika hospitalini hapo, ambapo Shekhe Ponda alibebwa katika gari dogo lililokuwa na askari kanzu.
Askari hao walifika hospitalini hapo mapema na muda ulipowadia, walitoka naye na kumsaidia kupanda gari na kwenda naye Segerea.
Pamoja na Moi kukiri kuwa Ponda amepata nafuu kiasi cha kuruhusiwa, msemaji wa familia yake, Isihaka Rashid, alidai ndugu yake hajapata nafuu.
“Shekhe Ponda bado alikuwa mgonjwa, hatuelewi kwa nini wamemtoa hospitali,” alisema Rashid.
Juzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilihamia kwa muda Moi, katika wodi alimolazwa Shekhe Ponda na kusomewa mashitaka ya kuhamasisha vurugu maeneo tofauti nchini.
Ponda akiwa katika wodi maalumu, alisomewa mashitaka hayo na Mwendesha Mashitaka, Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa.
Hata hivyo, waandishi wa habari hawakuruhusiwa na Polisi kuingia katika chumba hicho. Lakini taarifa zilizopatikana kutoka katika ‘mahakama’ hiyo, kesi dhidi yake itatajwa Agosti 28.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, ambayo waandishi wa habari walipewa na Wakili wa Shekhe Ponda, Juma Nassoro, kiongozi huyo anadaiwa kutenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Juni 2 na Agosti 11, katika maeneo ya Zanzibar, Dar es Salaam na Morogoro.
Akizungumza nje ya chumba cha muda cha Mahakama hospitalini hapo, Wakili Nassoro alidai kuwa watapinga mashitaka hayo, kwa kuwa baadhi ya siku zilizotajwa zina utata, ikiwemo Agosti 11 aliyodai kuwa siku hiyo alikuwa amelazwa hospitalini akiuguza majeraha.
“Tumepanga kwenda kupinga mashitaka hayo siku ya kusikilizwa kwa kesi hiyo…ukiangalia hati ya mashitaka utabaini upungufu wa mambo mengi, na kwa bahati mbaya wakati akisomewa mashitaka hayo, sisi hatukuwa kwenye chumba hicho,” alidai Wakili Nassoro.
Kwa mujibu wa madai ya Wakili huyo wa Ponda, kesi hiyo ilisomwa muda mfupi baada ya wao kutoka nje ya hospitali, kwa kudhani siku imepita.
Alidai pia mashitaka yalisomwa kwa mteja wake, muda ambao saa za kazi zilikuwa zimekwisha, hatua aliyodai kuwa ni ukiukaji wa sheria na wanajiandaa kutumia hoja hiyo kupinga mashitaka hayo.
Hata hivyo, baada ya mashitaka hayo kusomwa na mtuhumiwa kukana, Wakili Nassoro alidai aliomba mteja wake asiondolewe hospitali hapo, kwa kuwa hali yake bado si nzuri.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini, limetuma timu ya wataalamu kwenda Morogoro, kuchunguza vurugu zilizotokea kati ya Polisi na wafuasi wa Ponda.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Polisi, Advera Senso, alisema timu hiyo ya uchunguzi, imeshawasili Morogoro na kuanza kazi.
“Kwa mujibu wa utaratibu wa Polisi, kutuma timu ya uchunguzi Morogoro ni sahihi na inapaswa kuchunguza nini kilitokea ili kupata ukweli,“ alisema Senso. “Tunataka kujua kama risasi zilifyatuliwa, kwa nini na ilikuwa katika mazingira gani.”
Alisema uchunguzi huo, hautaingilia kesi iliyopo mahakamani dhidi ya Ponda, na kutaka umma wa Watanzania kutulia wakati uchunguzi huo, ukiendelea.
Katika hatua nyingine, Senso alisema polisi inamshikilia askari polisi aliyepiga risasi juu siku ya tukio la jaribio la kumkamata Shekhe Ponda mjini Morogoro kwa uchunguzi.Jina la polisi huyo halikutajwa.
0 comments:
Post a Comment