Akitoa maelezo yake jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Rehema anasema
kutokana na kazi hiyo alikuwa akilazimika kufanya ngono zembe ili
kujiongezea kipato. Hata hivyo, anashukuru Mungu hakupata maambukizi ya
Ukimwi.
“Wakati tukifanya kazi hiyo, mimi na wenzangu tulikuwa tukifanya ngono
zembe, hasa na madereva wa magari ya mizigo yanayoegeshwa karibu na baa
tulizokuwa tukifanyia kazi,” alisema Rehema.
Hata hivyo, Rehema sasa ameachana na kazi hiyo na amepata msaada kutoka Shirika la Kazi duniani (ILO).
“ILO walikuja Njombe na kutushauri tuunde vikundi ambapo tulipewa fedha
zilizotuwezesha kufanya kazi zenye staha. Sasa ninauza nguo sokoni na
ninapata fedha za kutosha kutokana na biashara hiyo. Tumeanzisha
ushirika wa kuweka na kukopa (Saccos) ambayo inatuwezesha kujiendeleza
kiuchumi,” anasema.
Kwa upande wake Mwajuma Sabuni anayefanya kazi katika kiwanda kimoja
jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) analalamikia unyanyasaji wa
kijinsia kutoka kwa waajiri wao.
“Nimefanya kazi katika kiwanda hiki kwa miaka saba sasa. Kwa miaka
miwili ya awali nilifanya kazi kama kibarua, lakini baadaye nikaingizwa
kwenye mkataba wa kazi na kuanza kukatwa mafao ya uzeeni na Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF), bila kupewa kadi ya uanachama na mwajiri wangu.
Hadi sasa sijui hatima ya pensheni yangu,” anasema na kuongeza:
“Kwa jumla hali ya ajira katika kiwanda hiki ni ngumu hasa sisi
wafanyakazi wa kike kwani rushwa ya ngono iko nje nje. Wasimamizi wa
vitengo ndiyo wahusika na ukiwakataa ajira yako inakuwa hatarini. Licha
ya kuwepo kwa Chama cha Wafanyakazi (Tuico) kinachojua kero zote hizi,
bado hazijashughulikiwa. Naiomba Serikali iingilie katika kwa kuchunguza
madai haya kwani tunanyanyasika mno.”
Maelezo ya wanawake hawa yanawakilisha kilio cha wafanyakazi wengi
wanaonyanyaswa kijinsia kutokana na kazi zao. Wengi hulazimika
kujiingiza kwenye ngono zisizo salama, hivyo kuhatarisha maisha yao hasa
kwa kupata ugonjwa wa Ukimwi.
Katika mkutano wa wadau wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, hasa maeneo
ya kazi uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wadau wanasema
kuwa wanawake na wasichana wako kwenye hatari zaidi ya kuathirika na
ugonjwa huo na kwamba hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa ili kukabilia
na tatizo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk
Fatma Mrisho anasema kuwa makundi ya wanawake walijitokeza kuomba msaada
ili kujikwamua kimaisha na kujilinda.
“Hatari ya wanawake hawa kuathirika na Ukimwi ni kubwa mno. Ni
changamoto kubwa inayohitaji jitihada za kila mmoja wetu,” anasema Dk
Mrisho.
0 comments:
Post a Comment