Thursday, 27 June 2013

FILAMU MPYA YA AUNT EZEKIEL YAZUILIWA BAADA YA KUWA NA VIPANDE VYENYE KUCHOCHEA NGONO




SERIKALI kupitia bodi ya filamu nchini imemkalia kooni mwigizaji, Aunt Ezekiel na kumtaka aondoe baadhi ya vipande vya sinema yake mpya iitwayo Scola vinginevyo haitaruhusiwa kuingia mtaani.


Taarifa kutoka ndani ya bodi hiyo inayosimamia maadili ya sinema za Kitanzania, imeeleza kuwa Aunt aliipeleka  filamu hiyo ili ikakaguliwe kama zilivyo taratibu lakini bahati mbaya ikagundulika kuna ‘sini’ tatu ambazo zilitoka nje ya maadili ya mtanzania.


“Kuna vipande vitatu ambavyo kimsingi vimevuka matakwa ya maadili ya Kitanzania hivyo hakuna jinsi, lazima avitoe kama anataka kuiingiza sokoni sinema hiyo,” kilieleza chanzo makini ndani ya bodi hiyo kilichoomba hifadhi ya jina.

Kabla ya mwandishi wetu hajazungumza na Aunt, alimpata rafiki wa karibu na staa huyo ambaye alifafanua kuwa rafiki yake (Aunt) amekaliwa kooni na bodi hiyo lakini bado yupo katika mazungumzo kuona kama anaweza kuruhusiwa aendelee.
 

“Amejaribu kuwasihi ili kama kuna uwezekano iingie mtaani pasipo kuviondoa hivyo vipande kwani navyo vina umuhimu wake,” alisema rafiki huyo wa Aunt kwa sharti la kutochorwa jina gazetini.


Alipotafutwa Aunt kuhusiana na suala hilo, alikiri kukaliwa kooni na bodi na kuomba apewe muda wa siku mbili ili aweze kulitolea ufafanuzi suala hilo lakini hakufanya hivyo, badala yake akasafiri nje ya nchi.


Mwaka jana mwishoni, bodi hiyo ya filamu ilimzuia mwigizaji Vincent Kigosi ‘Ray’ kuingiza sokoni sinema ya Sister Mary baada ya kuridhishwa na madai ya Kanisa Katoliki yalioainisha kuwa asilimia kubwa vipande vya sinema hiyo vilidhalilisha Ukatoliki.

0 comments:

Post a Comment