Wakati Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Arusha, Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao watawasili
Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama kwenye
msiba huo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja
vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza
uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao
watasafirishwa.
Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa
habari, alisema taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la
kutupwa kwa mkono (grumeti) na hivi sasa timu ya wataalamu ikiongozwa
na Kamishna wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja
inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema katika taarifa
yake kwa vyombo vya habari ameahidi kupambana na kuhakikisha wahusika
wanapatikana.
Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es
Salaam na kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo
ni wawili na 68 ni majeruhi.
Waliokufa ni Katibu wa Baraza la
Wanawake (Bawacha) wa Chadema, Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na
mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin.
"Mpaka hivi sasa watu
waliokufa ni wawili na wengine 68 wamejeruhiwa na mlipuko huo, lakini
naahidi kuwa tutapambana na kuhakikisha tunawapata wahusika," alisema
Mwema.
Sanjari na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa bomu, Mwema
alisema timu ya jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda Arusha
kuongeza nguvu katika upelelezi.
Hata hivyo, hakufafanua zaidi juu
ya mtuhumiwa huyo kutokana na kile alichosema taarifa husika
zinafanyiwa uchunguzi kabla ya kuwakamata watu sahihi waliohusika na
tukio hilo.
Kwa mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao
Makuu inayoongozwa na makamishna wawili, imeondoka kwenda mkoani Arusha
kuongeza nguvu katika operesheni na upelelezi.
Timu hiyo inaongozwa
na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Isaya Mngulu
kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, wakishirikiana na vyombo
vingine vya ulinzi.
Alisema polisi inafanya operesheni kali nchini
kote kuhakikisha inawatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili
na waliotenda uhalifu huo.
"Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea," alisema.
IGP
ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za wahalifu hao, atoe taarifa
kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo
chochote cha polisi ili wakamatwe.
‘Kwa nini iwe Arusha’ hii ni
kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mulongo aliyoitoa baada ya kutembelea
majeruhi katika Hospitali za Mount Meru, St Elizabeth pamoja na
Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre jijini.
“Nawapa pole
sana ndugu zangu wa Chadema, na wana Arusha kwa ujumla pamoja na
watanzania. Lakini najiuliza kwa nini Arusha …tukio hili limenihuzunisha
sana na nawaomba tusiingize masuala ya kisiasa, tuache polisi
wachunguze tukio hili kwani timu ya wataalamu kutoka Jeshi la Ulinzi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na wataalamu wengine wanachunguza tukio
hili na wahusika watachukuliwa hatua.’’
Mulongo ambaye tukio hilo la
juzi limekuja ikiwa ni mwezi mmoja tangu kutokea kwa mlipuko katika
Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi la Olasiti, alisema jana anayefanya
ulipuaji wa mabomu na kumwaga damu za watu mbalimbali na wengine kufa,
ipo siku Mungu atamhukumu.
Kati ya majeruhi 59 waliolazwa kwenye
hospitali hizo, wawili wamehamishiwa Hospitali ya KCMC kutoka Hospitali
ya AICC kwa matibabu. Wagonjwa wengi wamelazwa hospitali ya Selian
ambao ni 40. Hata hivyo, wanane waliruhusiwa baada ya matibabu.
Mkuu
wa Mkoa alisema anajisikia mnyonge kutokana na matukio hayo mawili
tofauti; mlipuko wa kanisani na la juzi wakati Chadema ilipokuwa
ikihitimisha kampeni zake za udiwani kwenye kata nne za Themi, Kaloleni,
Elerai na Kimandolu ambao hata hivyo uliahirishwa kutokana na tukio
hilo.
Mulongo alitaka wananchi wasihusishe na masuala ya kisiasa
badala yake wawaachie polisi kuchunguza tukio hilo. Kwa mujibu wa
Mulongo, watu kadhaa wamekamatwa.
Katika kipindi kisichozidi miezi
miwili, mji wa Arusha umeshuhudia majeruhi wasiopungua 130, na vifo vya
watu watano vilivyotokana na kurushwa mabomu na watu wasiojulikana
katika mikusanyiko kanisani na kwenye mkutano huo wa siasa wa Chadema.
Katika
tukio la mwezi uliopita katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi, watu watatu walifariki na wengine wapatao 59 kujeruhiwa.
Mmoja wa watuhumiwa ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda,
Victor Ambrose alifikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika katika
shambulio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, daktari wa
hospitali ya Selian, Paul Kisanga alisema walipokea wagonjwa 48 kabla
ya wanane kuruhusiwa.
Alisema miongoni mwa wagonjwa hao, wamo watoto
watano wanne wakiwa wa kiume na mmoja wa kike. Mtoto Fahad Jamal (7)
amelazwa kwenye wadi ya wagonjwa mahututi chini ya uangalizi wa
madaktari.
Hospitali ya St Elizabeth wapo wagonjwa wanane na Mount
Meru imepokea wagonjwa tisa. Mganga Mkuu wa Mkoa wa hospitali ya Mount
Meru, Frida Mokiti alisema wamepokea miili ya marehemu wawili ambao ni
Judith Moshi (25) ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) kata
ya Sokoni 1, Jijini Arusha pamoja na mtoto aliyejulikana kwa jina moja
la Justin (13).
Kwa mujibu wa majeruhi wa tukio hilo, Abraham
Samuel waliona kitu kikiwa kwenye mfuko wa rambo kikirushwa juu na baada
ya muda mfupi walisikia vilio na wengine kuzimia.
Kitu hicho
kilirushwa kabla ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Taifa, Freeman
Mbowe kuhitimisha kampeni za uchaguzi za udiwani wa kata nne za Jimbo la
Arusha Mjini.
Mlipuko huo unadaiwa kuwa ulitokea jirani na gari la
matangazo la Chadema, aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa karibu na
jukwaa alilokuwa akitumia Mbowe.
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe amedai tukio hilo si la bahati mbaya bali lilipangwa na kundi la watu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, alisema wabunge wa chama hicho leo
hawataingia bungeni bali watawasili jijini Arusha kwa ajili ya kuungana
na wananchi pamoja na wanachama wa kwenye msiba huo.
Kwa mujibu wa
Mbowe, marehemu Judith atapelekwa mkoani Kilimanjaro na Justin
atapelekwa mkoani Tabora kwa ajili ya maziko mara baada ya polisi
kukamilisha uchunguzi juu ya tukio hilo.
Alisisitiza kwamba kuanzia
leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba
huo na mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo
hivyo marehemu hao watasafirishwa.
‘’Nimetembelea majeruhi jana
hospitalini lakini kwa Hospitali ya Selian, Arusha Lutheran Medical
Centre majeruhi ni wengi lakini walioumia sana ni watoto kuna mtoto
mmoja amekatika mkono na mguu ambaye ni Sharifa Jumanne na Amiri Ally
ana vyuma vitatu mwilini mwake,’’ alisema Mbowe.
Ingawa polisi
imesema inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kutoa taarifa
kamili, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kwamba zipo taarifa kwamba
shambulio hilo liliambatana na risasi za moto.
Chama cha Wananchi
(CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, kimelaani
tukio hilo na kutaka Serikali ichukue hatua za haraka na kukamata
waliohusika na matukio hayo iwe fundisho.
“Hatuna sababu na tusijenge
utamaduni wa nchi yetu kugeuka eneo ambalo palipo na mkusanyiko mabomu
yanalipuka, Tanzania ni nchi ya amani, kwa matukio haya CUF tunalaani
kwa nguvu zote na kutoa pole kwa familia zilizoathirika,” alisema
Lipumba.
Lipumba alisema kitendo kilichofanyika katika mkutano huo wa
Chadema ni unyama wa kutisha wenye makusudi ya kundi fulani kutekeleza
azma yao dhidi ya chama, watu, kundi na viongozi.
Alisisitiza kuwa
utamaduni huo wa kufanya unyama katika mkusanyiko wa watu unapaswa
kudhibitiwa mapema ili kuepusha madhara mengine ndani ya jamii kwa
kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na familia tegemezi.
“Tumefikia
hatua mbaya sana ya kufanya siasa za mabomu huu ni utamaduni unaopaswa
kukemewa na kupingwa, matukio haya yanajirudia kutokana na Serikali
yenyewe kuyakaribisha kwa kushindwa kuwachukulia hatua kali wahusika,
tunaomba dola ifanye ifanyalo katika uchunguzi wake na kuwakamata na
kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment