Majuto anasema kuwa ana watoto tisa ingawa hakuwa tayari
kuwazungumzia mama wa watoto hao zaidi ya kumwongelea mkewe wa sasa,
Aisha Mbwana kwa kuwa wake zake aliozaa nao baadhi ya watoto kwa bahati
mbaya walishafariki dunia.
Alisema kuwa yanapokuja masuala ya familia huwa
anapenda azungumze mkewe na kwa ridhaa yake. Kwa mujibu wa Majuto
anapenda aitwe mke halali kwa kuwa wake feki anao wengi kupitia michezo
ya kuigiza na wengine wenye fikira potofu hutumia picha hizo kutengeneza
habari za uongo.
Aisha anaizungumziaje familia yake
Kama kawaida ya wanawake wa Tanga ana lafudhi ya
huko ambayo huvutia kuzungumza nao, anaanza kwa kunieleza kuwa alianza
kuitwa mke halali wa nguli huyo wa sanaa za maigizo mwaka 1997,
walipofunga ndoa .
Anasema kuwa alikutana na nguli huyo maeneo ya
Buguruni, Dar es Salaam, ambako alikuwa akiishi na dada yake aliyekuwa
kaolewa na rafiki yake mzee Majuto, ‘Mwanachia’ (kwa sasa ni marehemu),
ambaye walikuwa wakiigiza pamoja.
Anasema hakuwa na hili wala lile hadi alipoamua
kuondoka na kurudi kwao maeneo ya Vingunguti, ambako ndiko walikokuwa
wanaishi wazazi wake na kupewa taarifa kuwa posa imepelekwa kwa ajili
yake.
“Nilipoambiwa kuhusu hiyo posa sikufikiria kama
atakuwa ni mzee Majuto kwa kuwa alikuwa ni kama shemeji yangu kutokana
na kuwa karibu na shemeji yangu,” anasema Aisha ambaye ni mama wa watoto
watatu.
Anaendelea kueleza kuwa siku ambayo wanafamilia
walikutana na kumuuliza kama anamfahamu mchumba na kutajiwa jina kuwa ni
Amri Athumani, aliuliza mara mbili kwa kuwa alikuwa hamfahamu huyo mtu
hadi alipoambiwa kuwa ni King Majuto.
“Kwa mila za Wabondei mchumba wa kwanza
anakubaliana na wazazi, halafu binti anapewa taarifa na kwa kuwa wazazi
ni wakubwa inabidi binti akubali, na ndivyo ilivyokuwa kwangu nikakubali
na kuolewa na Majuto,” anasema mama huyo.
Anaingia kwenye uigizaji kufuata nyayo za mumewe
Aisha anafafanuwa kuwa kabla ya kuolewa na Majuto
hakuwa mwigizaji lakini baada ya kuolewa, mumewe huyo alimwingiza kwenye
uigizaji na filamu ya kwanza kuigiza na mumewe huyo ni ‘Fukara
hatabiriki’.
Mkewe huyo anasema kipindi hicho Majuto alikuwa
anafanya kazi bila kuwa na kikundi zaidi ya wanafamilia, hivyo na yeye
alikuwa mmoja wao akicheza kama mama na Majuto kama baba.
0 comments:
Post a Comment