Friday, 13 September 2013

PADRI WA KANISA KATOLIKI ZANZIBAR AMWAGIWA TINDIKALI USONI...

  

Maeneo ya Mkunazini ambako tukio hilo lilitokea.
Matukio ya kushambulia watu kwa tindikali yameendelea kuitikisa Zanzibar, baada ya jana watu wasiojulikana kummwagia tindikali usoni Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mpendae, Anselmo Mwang'amba katika eneo la Mkunazini, Mji Mkongwe mjini hapa.

Padri Mwang’amba ni Mkuu wa Kituo cha Malezi kwa Vijana kilichopo Cheju wilaya ya Kati Unguja kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Zanzibar.
Tukio hilo ambalo limekuja mwezi mmoja tangu kumwagiwa tindikali kwa raia wawili wa kigeni waliokuwa wanafundisha kwa kujitolea  kisiwani hapa, zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis.
“Tumepokea taarifa ya tukio, lakini uchunguzi wa tukio hilo na kujua chanzo na mtandao wa wahalifu hawa umeanza,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa za daktari Abdallah Haidari wa hospitali ya Mnazi Mmoja ambako padri huyo alikimbizwa hapo baada ya kushambuliwa,   amejeruhiwa usoni na kifuani.
“Padri Mwang'amba amejeruhiwa usoni na kifuani kwa maji ambayo baada ya kuyafanyia uchunguzi tumegundua kuwa ni  tindikali,” alisema.
Akisimulia tukio hilo, Padri Mwang'amba alisema alishambuliwa na watu asiowafahamu  wakati akitoka katika duka linalotoa huduma za mtandao wa mawasiliano ya intaneti eneo la Sunshine, Mlandege katika majira ya jioni saa kumi.
“Wakati natoka katika duka kupata huduma za mawasiliano ya intaneti nilimwagiwa maji makali ambayo nilihisi kwamba ni tindikali na kuamua kwenda moja kwa moja katika hospitali ya Mnazi Mmoja,” alisema.
Mmoja wa wafanyakazi  wa duka linalotoa huduma za mawasiliano ya intaneti hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Salma, alikiri kutokea kwa tukio hilo ambapo mteja wake alipata huduma hapo.
“Wakati anatoka baada ya kupata huduma mara namuona anarudi na kulalamika kwamba amemwagiwa tindikali katika sehemu za uso,” alisema.
Hilo ni tukio la tano kwa watu mbali mbali kumwagiwa tindikali mjini hapa ambapo hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na ukatili huo.
Mwezi uliopita, walimu wawili wa kujitolea, raia wa Uingereza, kujeruhiwa kwa kumwagiwa tindikali, katika maeneo ya Mji Mkongwe, Shangani, Zanzibar. Walimu hao, Kate Gee (18) na Kristie Trup (18),  walivamiwa na kujeruhiwa saa moja usiku, wakienda kupata chakula cha jioni. Walikimbizwa Uingereza kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa muda katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment