WANAWAKE
wawili walioolewa katika familia moja ‘wake wenza’, mama Hashimu na
mama Fadhila, wakazi wa Kimara King’ong’o jijini Dar, hivi karibuni
walifikishwa serikali za mtaa kwa kosa la kutukanana matusi ya nguoni
pamoja na kushikana uchawi.
Inadaiwa kuwa wanawake hao ‘walimwagiana’ matusi hayo usiku wa manane
na kusababisha watu wengine kukosa usingizi na kukusanyika
kuwasikiliza.
Mara baada ya kufikishwa serikali ya mtaa, wake wenza hao walitakiwa
kueleza ugomvi wao na kila mmoja kuanza kushusha tuhuma kwa mwenzake.
Mapaparazi wetu waliwashuhudia wakati wake wenza hao walipokuwa
wakijieleza mbele ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa King’ong’o,
Demetrius Mapesi na Mtendaji wake Amina Rashid.
Mama Hashimu alianza kuelezea kisa kizima na kufuatiwa na mama Fadhila
ambaye wakati akijieleza alipandisha mori kiasi cha kumfanya atake
kumrukia mwenzake.
“Unajua nasikia hasira sana kwa sababu mama Fadhila ameniita mchawi huko
mtaani unadhani mimi nitaelewekaje? Ukweli kauli hiyo inaniuma sana,”
alisema mama Hashim na kuangua kilio.
Hata hivyo, baada ya kila mmoja kueleza ya moyoni, mwenyekiti wa
serikali za mtaa pamoja na mtendaji wake, waliwaamuru wake wenza hao
kupeana mkono na kuombana msamaha.
“Sasa hapa hakuna kesi, kwani wote mna makosa, hebu niambieni mnawafundisha nini watoto wetu kwa matusi
mliyotukanana hadharani?” alihoji mwenyekiti na kuwataka wayamalize mambo hayo.
Aidha, mwenyekiti huyo aliahidi kuwafuatilia ili kuona kama watakuwa wamebadili tabia zao.
Kama vile haitoshi aliwaahidi kama watarudia atawahamisha mtaa pamoja na
waume zao kwani mtaani kwao hawahitaji watu wanaotukanana ovyo na
kuzushiana mambo ya kichawi.
Baada ya tamko la mwenyekiti, mtendaji wake aliwaamuru wake wenza hao
kuandika matusi waliyotukanana kisha akawapiga faini ya shilingi 20,000
kila mmoja.
“Kutokana na matusi yenu nalazimika kuwapiga faini ya shilingi elfu
ishirini kila mmoja, ingawaje kwa mujibu wa sheria ya Tanzania mtu
akikutwa na hatia ya kutukana anatakiwa kutozwa faini ya shilingi elfu
hamsini au kufungwa jela miezi sita,” alisema mtendaji huyo.
Kila mmoja alilipa nusu ya faini na kuahidi kumalizia huku wakisema kuwa hawatarudia kufanya kosa hilo tena
0 comments:
Post a Comment