Ni umbali wa kilomita saba kutoka katikati ya Mji wa Dodoma upande wa
Mashariki barabara iendayo Morogoro, kipo kijiji maarufu cha Nzuguni.
Katika Mtaa wa maarufu wa Mapinduzi iko familia ambayo wakati
mwingine kwa mtu wa kawaida unaweza usiamini simulizi yake lakini ni
ukweli mtupu kwamba kuna tatizo katika familia hiyo jambo ambalo
linahitaji juhudi za makusudi kuwasaidia.
Waswahili wanasema ‘kama hujui kifo basi kachungulie kaburi’ hivyo
basi, hali ya maisha ya familia hii kwa ujumla inahitaji kusaidiwa,
wanaishi kwenye katika kibanda kidogo cha tope.
Ni katika familia ya Lameck Mwitewe Senyagwa na mkewe Anastazia Alfred
yupo Stephen Lameck (21), kijana ambaye hajui mwanga wa jua la kijiji
hicho ukoje, wala haijulikani ni lini kijana huyo ataishi walau kama
binadamu wengine.
Stephen (Leba) ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne wote
wakiwa wa kiume, lakini yeye pekee ndiye ambaye hajawahi kuyafaidi
maisha katika kipindi chote cha uhai wake.
Ni mlemavu wa miguu, mgongo na hazungumzi chochote ingawa kwa ishara anaweza kueleza nini anachotaka kutendewa wakati huo.
Kwa namna ilivyo, angeweza hata kuendesha baiskeli ya miguu mitatu,
lakini nani wa kumpa baiskeli hiyo ili imsaidie kijana huyo kuona mwanga
wa jua, ni tabu na mateso makubwa juu yake.
Nilifika katika kibanda kidogo ambacho familia hiyo ya watu sita (watoto
wanne na wazazi wawili wanaishi), inatia huruma lakini ndiyo hali
halisi waliyo nayo, na haikuwa mara ya kwanza kuona maisha duni kama
hayo isipokuwa mateso yapo kwa Stephen.
Simulizi ya mama mzazi
Katika kibanda hiki, nakutana na mama mzazi wa kijana huyu, mara baada
ya kujitambulisha anaonyesha ushirikiano, isipokuwa anapinga mimi
kuingia ndani huku akitaka historia ya kijana wake niipate nikiwa nje.
Baada ya dakika kadhaa tunakubaliana kuingia ndani aliko Leba.
Nilitaka kujua historia kamili na yeye alianza kwa kusimulia “Leba ni
mwanangu wa kumzaa, ndiye mtoto wangu mkubwa kati ya watoto wanne,”
anaanza kusimulia Anastazia Alfred.
Mama huyo anasema kuwa tatizo la kutokutembea kwa Leba halikumuanza hivi
karibuni, bali ni tangu alipokuwa tumboni na lilitokana na tatizo
alilokuwa nalo mama yake mzazi kabla ya kuzaliwa kwa mtoto.
Chanzo cha ulemavu
Anasema tatizo la mwanaye lilianza katika ugonjwa ambao yeye mzazi aliupata wakati akiwa na mimba ya miezi sita.
“Niliambiwa kuwa ninaumwa kifafa cha uzazi, wakati huo nilikuwa siwezi
kufanya jambo lolote na hata macho yangu yalikuwa hayaoni,” anasimulia
Anastazia.
Mama huyo anasema mara baada ya ugonjwa huo kumzidi, alipelekwa katika
hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambako alijifungua mtoto wakati huo akiwa na
mimba ya miezi saba.
Anasema baada ya kujifungua, mtoto alikuwa ni dhaifu kiasi kwamba wengi
walikata tamaa kuwa asingeliweza kupona. Hata hivyo kwa mapenzi ya Mungu
akapona.
Atoroka na kumwacha mtoto
Kwa maneno yake anasema kuwa alitoroka hospitalini na kwenda kwa ndugu
zake katika Mtaa wa Makole ambako aliwaeleza kuwa asingekuwa tayari
kuendelea kuishi na mtoto ambaye watu walishamwambia kuwa ni mkosi
kuishi naye.
Hata hivyo, alikumbana na changamoto nyingine kutoka kwa watu ambao
walimtaka arudi tena kwa ajili ya kumchukua mtoto na kwamba wasingekuwa
tayari kumpokea mahali popote kama angerudi bila ya Leba.
“Nilikuwa nimechanganyikiwa na wakati mwingine utoto ulikuwa bado
unanisumbua na kwa kuwa sikuwa na mama wakati huo ambaye angeweza
kunifunda zaidi hivyo nikaona njia njema ya kunisaidia ni kumtelekeza
mtoto,” anasimulia.
Hata hivyo, anampongeza marehemu baba yake kuwa alikuwa ni msaada mkubwa
kufanya mtoto huyo aendelee kuishi kwani aliposikia mambo hayo,
alimwita kijijini kwao Kwamtoro Wilaya ya Chemba (zamani Kondoa) ambapo
alimketisha chini na kumwonya juu ya tendo hilo.
Anasema baba yake huyo alimtaka kuishi na mtoto bila ya kumtenga, na
akampa mifano hai ya watu wenye ulemavu ambao wanaishi hadi wakati huo.
Mateso ya mtoto
Mbali na kukubaliana na kuishi na mtoto huyo, hali ya Leba kwa sasa
inatisha, hana msaada wowote. Hawezi kutoka nje, amekuwa akifichwa ndani
kwa zaidi ya miaka 12 sasa.
Chakula ni tabu, mazingira anayoishi hayaendani na hali yake na haijulikani ni lini atapata nafasi ya kuona mwanga.
Ni zaidi ya miaka 12 sasa kijana huyo anaishi ndani ya nyumba na watu
wengi hawamjui licha ya kuwa mama yake anajulikana kwa jina la Mama
Leba, mwenye jina majirani hawamjui.
Hiyo itatokana na kushindwa kupata msaada wowote walau wa baiskeli au
hata njia nyingine, zaidi ya kutegemea mama yake mzazi ambaye anasema
kuwa kijana huyo amekuwa mzito hawezi kumbeba.
Hali ya familia
Maisha ya familia ya Lameck ni magumu, hawana nyumba, wanaishi katika
kibanda kidogo ambacho wamepewa na mlo wao ni shida, humlazimu baba wa
familia kutafuta kwa bidii huku watoto wote watatu wakimtegema kwa
masomo mmoja akiwa kidato cha nne, mwingine amemaliza darasa la saba na
wa mwisho darasa la pili.
Hata hivyo, upendo wa kuwa pamoja bado umeendelea kuwafanya wasitupane wala kuwa na migogoro.
Nini wanahitaji
Anastazia anasema kama watapata nafasi ya kusaidiwa baiskeli kwa ajili
ya Leba akaweza kutoka nje, naye angepata nafasi ya kupumua na kutafuta
biashara yoyote ya kumsaidia mumewe kwani kwa sasa hawezi kutoka umbali
wa mita 100 na kumwacha mtoto.
Anasema katika umri wa miaka mitatu wa kijana huyo, walikutana na
mtaalamu kutoka Asia ambaye alisaidiana na wataalamu wa hospitali ya
mkoa kumfanyia mazoezi kijana huyo, kiasi cha kumwezesha kwa sasa
akipewa baiskeli anaweza kuendesha japo kwa shida.
Kwa sasa ni kama wamepoteza matumaini lakini wanaamini kwa misaada
kutoka kwa wasamaria wema labda hali ya maisha yao inaweza kubadilika na
kuwa nzuri zaidi ya ilivyo sasa.
-Mwananchi
0 comments:
Post a Comment