Baadhi ya silaha. |
Operesheni Kimbunga inayoendelea
kwa awamu ya pili, imebaini hifadhi haramu ya silaha za kivita, katika
kijiji bandia cha wahamiaji haramu cha Nyamgali kutoka Burundi,
kilichokuwa wilayani Kasulu.
Akizungumza na mwandishi aliyefika katika kijiji hicho juzi, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo, Danhi Makanga, alisema hifadhi hiyo ilikuwa kituo cha silaha zilizovushwa kutoka nchini humo.
"Hapa kilikuwa kituo cha silaha za kivita na mabomu ya kurusha kwa mkono vilivyovushwa kutoka Burundi na kupitishwa kwa njia za panya," alisema Makanga aliyekuwepo katika kituo hicho.
Hifadhi hiyo iliyojengwa mithili ya kituo cha kuhifadhi chakula, ipo katika kijiji hicho ambacho wahamiaji hao haramu wamejenga nyumba za kudumu za kuishi.
Mbali na nyumba za kudumu za kuishi, katika kijiji hicho, kuna shule zinazofundisha kwa lugha za Kirundi, Kifaransa na Kiingereza na maduka yakiwemo ya dawa baridi.
Pia zipo baa zinazouza vinywaji kutoka Burundi, makanisa, karakana za ufundi seremala na hata
mashine za kusaga.
"Watu wanakuja na kujenga himaya yao, tena kwa kuidharau nchi waliyohamia na kutumia hata fedha zao ndugu zangu, hapa ndipo palipokuwa mahali hatari mno," alisema Makanga.
Kutoka katika kituo hicho kwa mujibu wa Makanga, silaha zilisambazwa kwenda sehemu nyingine za nchi, hadi Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyamidaho, Ramadhani Shaaban, alisema aliogopa kufuatilia wahamiaji hao kwa kuwa walikuwa wakitoa vitisho kwa kutamka waziwazi kuwa wako tayari kuua watu watakaowafuatilia.
"Waliingia kwa ubabe na kutwaa ardhi na kujianzishia utaratibu wao, hawakutaka kusikia lolote na walioanza kuingia hapa ni wale waasi wa Burundi. Walikuwa na silaha na pia hapa ilikuwa njia yao kuu ya kusafirisha silaha.
"Kwa kuwa walikuwa tishio kwa usalama wa wakazi wa Mvugwe na maeneo jirani, tulitoa taarifa ngazi za juu, taratibu za kuwaondoa zikaanza na wakati mambo yameiva, likaja agizo la Rais Jakaya Kikwete.
"Tunashukuru adha hii inatuondoka sasa," alisema Shaaban na kuongeza kuwa, pamoja na kuishi kinyume cha sheria, waliongoza kwa kulima bangi katika eneo hilo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, aliwahimiza Wana-Kigoma kutowalinda wahamiaji haramu, huku akisisitiza kuwa kamwe hatakubali kuona Warundi wanageuza Mkoa wa Kigoma kuwa maficho ya wahalifu.
Aliahidi kushirikiana na viongozi wa ngazi zote mkoani Kigoma kuendesha msako wa mara kwa mara dhidi ya wahamiaji haramu.
Tangu kuanza kwa Operesheni Kimbunga, zaidi ya raia 4,365, wamekamatwa na kurejeshwa nchini mwao, achilia mbali walioondoka kwa njia za panya.
Operesheni Kimbunga ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya uhalifu vilivyokithiri vikiwemo ujambazi wa kutumia silaha, ujangili, utekaji wa magari na mauaji ya kikatili pamoja na migogoro ya ardhi inayotokana na wafugaji kutoka nchi jirani kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho.
Rais Kikwete alitoa agizo la kuanza kwa operesheni hiyo Julai 29, 2013 akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera.
Katika agizo hilo, alitaka kufanyike operesheni maalumu ya kuondoa wahalifu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita, ambao kwa kiasi kikubwa wengi ni wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.
Operesheni Kimbunga inayoongozwa na Brigedia Jenerali Mathew Sukambi, ilianza Septemba 6, 2013, baada ya kupita wiki mbili alizokuwa amezitoa Rais Kikwete alipowataka wahamiaji wanaoishi nchini bila kufuata sheria, kuondoka kwa hiari yao au kuhalalisha ukazi wao nchini.
0 comments:
Post a Comment