Tuesday, 25 June 2013

MAMA AMWAGA MACHOZI BAADA YA KUJIFUNGUA MAPACHA WALIOUNGANA NA WANATUMIA NJIA MOJA YA HAJA KUBWA


MWANAMKE mmoja mkazi wa Kijiji cha Kasumuru, Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Grace Joel Lwesha (19), amelia baada ya kujifungua watoto walioungana.


Akizungumza na waandishi wetu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jengo la Watoto, Grace alilia kutokana na kile alichodai kujifungua watoto walioungana wakati yeye ni maskini.


Watoto hao mapacha wa kiume, Eliudi na Elikana wameungana sehemu ya makalio hivyo kulazimika kutumia sehemu moja ya haja kubwa.
 

Grace aliwaambia waandishi wetu kwamba, watoto hao walizaliwa katika Hospitali ya Kyela, Februari 20, mwaka huu wakiwa na miguu miwili na mikono miwili kila mmoja.
 


“Baada ya kujifungua Machi mosi nilihamishiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kwa uchunguzi zaidi ili waweze kujua ni jinsi gani watakavyotenganishwa,” alisema.


Hata hivyo, hospitali hiyo ya mkoa haikufanikiwa badala yake Machi 16, walimhamishia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo kuanzia hapo mpaka sasa anafanyiwa maandalizi kwa ajili ya safari ya kupelekwa nchini India kwa upasuaji.
 

 “Ninawapenda sana watoto wangu hawa pamoja na kwamba wapo katika hali hii, ndugu zangu walipokuja hospitalini kuniona akiwema mama yangu walinifariji na kunisihi nisiwachukie nizidi kuwapenda.
 

“Kuwatunza ni kazi ngumu sana kwani mara nyingi wamekuwa wakininyima usingizi kwa sababu wamekuwa wakilala kwa nyakati tofauti.
 

“Nakumbuka siku niliyojifungua mume wangu alikosa raha lakini sasa anawapenda kwani amejua kuwa hii ni zawadi kutoka kwa Mungu.
 

 “Maisha yetu ni magumu kwani tunatoka kwenye familia maskini, kazi yetu ni kilimo cha kutumia jembe la mkono hivyo bado kuna mahitaji mengi nashindwa kumudu. 


Nichukue nafasi hii kuwaomba msaada Watanzania wote walioguswa na tukio hili,” alisema Grace.
 

Grace alifunga ndoa na Erick William Mwakyusa Desemba 23, 2010 na katika ndoa yao wamejaliwa kupata mtoto mmoja aitwaye Lide (3) na hao mapacha ni uzao wake wa pili.

Mama huyo anaomba msaada kwa mtu yeyote aliyeguswa na habari hii atume mchango wake kupitia namba 0753308525 ambayo ni ya mumewe au aende kumuona Muhimbili.

0 comments:

Post a Comment