Childress ni msaidizi wa Obama katika Ikulu ya
Marekani (White House) akiwa Naibu Mkuu wa Utumishi anayeshughulikia
mipango katika Serikali ya nchi hiyo na aliwahi kufanya kazi katika
Bunge la Seneti.
Obama amefanya uteuzi huo ikiwa ni wiki moja tangu
alipohitimisha ziara yake katika nchi tatu za Bara la Afrika, Tanzania
ikiwa mojawapo. Pia alizitembelea Senegal na Afrika Kusini.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ikulu ya
Marekani jana ilisema nafasi hiyo inahitaji kuidhinishwa na Bunge la
Seneti la nchi hiyo. Uteuzi wake unaweza kuwa na maana kubwa katika
kutekeleza sera za nje za Marekani.
Katika miaka ya karibuni, Tanzania imeshuhudia
ziara za viongozi wakuu wa nchi hiyo nchini ambao ni Bill Clinton,
George Bush na Obama.
Kuteuliwa kwa Childress, kunaashiria kwamba Balozi wa sasa wa Marekani nchini Alfonso Lenhardt anakaribia kumaliza muda wake.
Awali, Childress ambaye aliwahi kuwa msaidizi na
msiri wa muda mrefu wa Seneta wa zamani, Tom Daschle, alitarajiwa
kushika moja ya nyadhifa mbili katika utawala wa Rais Obama ambazo ni
Mkuu wa Utumishi katika Idara ya Huduma ya Afya ya Jamii (HHS) au Naibu
Mkurugenzi katika Ofisi ya Maboresho ya Afya katika Ikulu ya Marekani.
Hata hivyo, jina lake liliondolewa katika
mapendekezo ya uteuzi wa kuongoza ofisi hizo baada ya kuhusishwa katika
masuala ya kodi Februari 2009, hivyo kubaki pasipo na jukumu maalumu.
Pamoja na mkanganyiko uliojitokeza awali kuhusu
majukumu yake, Childress alimudu kufanya kazi kubwa katika kuwezesha
kupitishwa kisha kutekelezwa kwa mabadiliko makubwa katika sekta ya afya
ya nchi hiyo. Aliteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Utumishi wa Marekani, 2012.
Mwaka 2009, mpigania mabadiliko na maboresho ya
sekta ya afya Marekani ambaye sasa ni Seneta, Edward M. Kennedy
alimwomba Childress kujiunga na timu yake ya ushauri wa masuala ya afya,
elimu, wafanyakazi na pensheni.
Timu hiyo pia ilikuwa na kazi ya kumshauri kuhusu
masuala ya mabadiliko ya afya na Childress alikuwa miongoni mwa watu
walioshiriki kutoa rasimu ya kwanza ya muswada wa Sheria ya Mabadiliko
ya Afya 2009.
Baada ya muswada huo kupitishwa Februari 2010,
Childress aliondoka katika kamati hiyo na kujiunga na Idara ya Huduma ya
Afya ya Jamii Marekani ambako alikuwa na wajibu wa kusimamia
utekelezaji wa sheria hiyo mpya akiwa Kaimu Msimamizi Mkuu wa idara
hiyo.
0 comments:
Post a Comment