Msanii wa filamu Tanzania, Agnes Gerald 'Masogange' alikamatwa na dawa za kulevya Afrika Kusini hivi karibuni. |
Serikali imeamua kuanza kuchapisha magazetini picha na majina ya wahusika wa biashara ya dawa za kulevya.
Hatua hiyo iliyotangazwa jana na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe inalenga kuisafisha nchi dhidi ya uchafuzi unaotokana na tatizo hilo.
Sambamba na kutoa msimamo huo, Dk Mwakyembe jana aliwaambia waandishi wa habari taarifa ya kukamatwa kwa mtuhumiwa wa dawa hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.
Mtuhumiwa huyo Edwin Monyo (39) mwenye pasipoti namba AB 202513 anadaiwa kukutwa na kete za heroin 86 na misokoto ya bangi 34, juzi usiku akisafiri kwenda Italia kupitia Zurich, Uholanzi.
“Dawa hizo zilikuwa ndani ya begi dogo alilohifadhi katika begi kubwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Waziri alikuwa akizungumzia ziara ya ghafla aliyofanya JNIA juzi kwa lengo la kujiridhisha kuhusu vifaa na taratibu zinazotumika kwa ukaguzi wa abiria, ili nchi isiwe kichochoro cha kupitisha dawa za kulevya.
Kuhusu kuchapisha majina na picha, alisema Serikali itakuwa ikifanya hivyo, ili wahusika wafahamike na hatimaye kukomesha biashara hiyo.
Hata hivyo, alisema leo atatoa taarifa juu ya Watanzania wawili waliokamatwa Hong Kong wakiwa na dawa kama hizo.
“Niliahidi kutoa taarifa juu ya tukio la Mtanzania aliyekamatwa na dawa hizo hivi karibuni katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini, lakini tukabaini kuna wawili wengine waliokamatwa Hong Kong … sasa hatutaji jina bila kuonesha picha,” alisema Dk Mwakyembe.
Kuhusu tukio la juzi, alisema mtuhumiwa alikamatwa saa 2:15 usiku ambapo alikuwa akitarajia kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uswisi na kwamba tiketi na hati yake ya kusafiria vinashikiliwa.
Alisema kwa hatua za ziada, Serikali itaanza utaratibu wa kumulika mizigo yote itakayokuwa inaingia nchini ili kuhakikisha kelele za dawa za kulevya zinamalizika.
Katika hatua nyingine, Dk Mwakyembe aliitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuwapandisha daraja na kuwaongeza mishahara watumishi wawili wa kike waliowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Alisema katika ziara yake ya ghafla alibaini kuwapo taratibu zote zinazotakiwa na kusema tatizo ni watendaji wanaopewa dhamana ya kusimamia ambao hawatekelezi wajibu wao kikamilifu.
Mwezi jana wanawake wawili raia wa Tanzania walikamatwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo, Johannesburg, Afrika Kusini, wakidaiwa kuingiza shehena ya dawa za kulevya zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6.8 wakitoka nchini.
Kamanda wa Polisi wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey Nzowa, aliwataja watuhumiwa hao ambao inadaiwa walishafikishwa mahakamani nchini humo kuwa ni Agnes Gerald 'Masogange' na Melisa Edward
0 comments:
Post a Comment