Thursday, 29 August 2013

WAHAMIAJI HARAMU 21,192 KUTOKA MIKOA MITATU WAONDOKA NCHINI...

Wahamiaji haramu.
Wahamiaji haramu 21,192 kutoka mikoa mitatu nchini, wameondoka kwa hiari yao kurejea kwao  katika kipindi cha mwezi mmoja tangu Serikali itoe agizo la kutaka waondoke.

Pamoja na uwepo wa vituo rasmi 78 vya Uhamiaji nchini, Serikali iliruhusu wahamiaji hao haramu kupita kwenye vituo rasmi na visivyo rasmi ili kurahisisha kuondoka kwao katika maeneo walimokuwa wakiishi.
Aidha, Idara ya Uhamiaji imetoa onyo kwa wananchi kutothubutu kuhifadhi wahamiaji hao, kwani operesheni ya kuwaondoa kwa lazima itakapoanza, haitachagua mkoa wa msako na itamkamata mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuhifadhi wahamiaji hao.
Kwa mujibu wa Idara hiyo, kati ya wahamiaji 21,192, Burundi inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waliorejea kwa hiari ambao ni 14,371 ikifuatiwa na Rwanda 6,411, Uganda 306, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) 84 na Zambia 20.
Hatua hii ya kuondoa wahamiaji hao na kuwarejesha kwao, ilianza mwishoni mwa Julai baada ya agizo la Rais Jakaya Kikwete alipokuwa ziarani mkoani Kagera na kubaini changamoto zinazoukabili mkoa huo zinazotokana na uwepo wa wahamiaji haramu.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alinukuliwa akisema kutafanyika operesheni kubwa ya kushitukiza ya kuwaondoa kwa lazima wahamiaji hao nchini. Jana Uhamiaji ilisema itahusisha mikoa yote hasa ya pembezoni na mijini ambako baadhi wamekimbilia.
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Abbas Irovya akitoa taarifa ya hatua hiyo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam, alisema mpaka sasa wahamiaji haramu 21,192 wameshaondoka kuanzia Julai 29 hadi juzi.
“Tunatoa angalizo kwa kila mgeni anayeishi nchini bila utaratibu atumie fursa hii kuondoka, popote walipo wasijidanganye kuhama maeneo waliko wakitarajia watajificha, Idara imejipanga saa 24, usiku na mchana, naomba wananchi wasiwahifadhi, operesheni haitachagua mwenye kosa kama ni raia au la,” alisema Irovya.
Akifafanua, alisema Idara imeweka vizuizi dhidi ya wahamiaji hao kutoka sehemu moja kwenda nyingine, na wananchi wanapaswa kujua kuhifadhi mhamiaji ni kosa la jinai na wanaojidanganya  wamehama, watakumbwa na operesheni ambayo itakuwa hatari kwao.
Mchanganuo wa kurejea kwao aliotoa Irovya, unaonesha kuwa, katika kipindi hicho, wahamiaji haramu 10,802 waliondoka Kagera kupitia vituo vinane. Kati yao waliorejea Rwanda ni 6,411, Burundi 4,085 na Uganda ni 306 jumla wakiwa 10,802.
Aidha, Kigoma jumla ya vituo visivyo rasmi vitatu kupitia kata za Nyamugari, Kitanga na Herushingo wilayani Buhigwe, vilihusika kupitisha wahamiaji Warundi 10,128 na vituo rasmi vinne vilitumiwa na wahamiaji 144 kati yao Wakongo wakiwa 20 na Warundi 124.
Irovya alisema Rukwa, vituo vinne vinne vya Kirando, Kabwe, Kasanga na Wampembe vilihusika na jumla ya waliorejea kwao ni 118. Alisema 64 walirejea DRC, 34 Burundi na 20 Zambia.
Alipoulizwa sababu za Uhamiaji kutumia vituo visivyo rasmi na hatua ya kurejea kutohusisha mikoa mitatu pekee, wakati Tanzania imepakana na nchi nane, Irovya alisema nchini kuna vituo 78 vya kutoka na kuingia na visivyo rasmi na visivyo na ofisi za Idara hiyo, lakini watumishi wapo katika kata kufuatilia uhamaji huo.
Kuhusu mikoa mitatu, Irovya alisema, “Si kwamba kwingine hawapo, la, ila mikoa hii mitatu imekuwa na matukio mengi zaidi ya ujangili, utekaji, ujambazi na uharamia wa kutisha yanayosadikika kufanywa na wahamiaji haramu, lakini operesheni itahusisha nchi nzima”.
Alisema wahamiaji hao huingia nchini kama wafugaji wanaoingiza mifugo kulisha na kisha kuhamia, wengine hukimbia vita na machafuko huku wengine wakiingia kutafuta kazi na biashara kinyume cha utaratibu, hao wamekuwa wakimiliki ardhi na kukaa nchini kinyume cha sheria.
“Kuna utaratibu wa kukaa nchini kwa kila mgeni, sheria zinapaswa kuzingatiwa na kufuatwa, kama kuna Ofisa Uhamiaji anapatikana na hatia yoyote ya kupokea rushwa ili wahamiaji hawa wasiondoke, aripotiwe katika chombo cha usalama cha karibu na hatua kazi zitachukuliwa,” alisema Irovya akijibu swali kuhusu malalamiko ya wananchi kwamba baadhi ya maofisa uhamiaji wanapewa rushwa kuwaficha wahamiaji hao.

0 comments:

Post a Comment