TUNAENDELEA na mada yetu ambayo lengo lake la juu kabisa ni kukutaka utulie kwenye upendo wako. Huwezi kuishi na mwenzi wako katika mazingira ambayo ni tambarare kila siku, zipo nyakati ambazo mambo hayatakwenda sawa lakini hiyo haina maana kuwa hampendani.
Kuna mambo ya kujiepusha nayo, wiki iliyopita nilifafanua kipengele kuhusu hasira kwamba ni vizuri kuzidhibiti, siyo unatofautiana kidogo na mwenzi wako lakini unamkasirikia utafikiri ameua mtu. Hilo ni kosa kubwa.
Nilitoa mfano wa Scholastica na Romy, kwamba mrembo huyo alisikia maneno kuhusu mchumba wake ni msaliti, akamkasirikia na kuamua kumuacha. Alipokuja kugundua alimhukumu mwenzi wake kimakosa, alijuta sana. Akatamani kurudi, kesho yake alipompigia simu akaambiwa Romy ni marehemu. Akalia sana, kwani mwenzi wake amekufa na kifundo, alimhukumu bila hatia.
Mpaka hapo utakuwa umejionea hasara za hasira. Kingine kutokana na mfano wa Scholastica ni kwamba linalowezekana leo lisingoje kesho. Pengine baada ya kuujua ukweli na kumpigia simu Romy wakati huohuo, wangeweza kuzungumza na kuombana radhi. Aliposema atafanya kesho, akakuta mwenzake ameshatangulia mbele za haki.
DHARAU
Unapotofautiana na mwenzi wako hakikisha humpuuzi hata kama jambo lenyewe ni dogo. Unaweza kudhani halina maana yoyote na ukaliacha bila zingatio lolote, huwezi kujua ndani yake anaumia kiasi gani. Muweke karibu halafu sawazisha dosari yoyote ile japo wewe unaiona ya kipuuzi.
Dharau yako inaweza kumfanya mwenzi wako ahisi upendo hakuna. Akaona unamnyanyapaa hata akaamua kuanzisha uhusiano na mtu mwingine. Kumbe wewe ndiye mwenzi wake wa dhati, mwenye mapenzi ya kweli. Hakikisha unajiweka mbali na dharau.
Kuna mifano hai ya watu walioachana kwa sababu ya dharau tu. Hakuna kosa kubwa ambalo mtu anaweza kulifanya kama kumdharau mwenzi wake. Uhusika wenyewe unakataza hilo. Inawezekanaje ukathubutu kumpuuza mtu ambaye anakupenda?
Je, unajua thamani ya mapenzi kweli? Elewa kuwa dharau yako haina nafasi kwake. Utakuja kukumbuka umuhimu wake baadaye. Nyakati hizo ameshachukuliwa na mtu mwingine ambaye anampenda. Inabaki inakuuma na unajutia nafasi ambayo uliipoteza. Majuto mjukuu.
Upande wa pili, wewe ambaye unahisi mwenzi wako anakudharau jaribu kupuuza vitu vidogo halafu shika ukweli ambao unawaunganisha. Anakudharau ndiyo lakini swali la msingi la kujiuliza ni hili, je, mnapendana? Kama jawabu ni ndiyo, basi shughulikia hilo tatizo la mwandani wako.
Kama hutashika ukweli kwa vipimo vyake, bila shaka utakimbilia kuachana naye kwa kuamini hilo ndilo suluhisho la matatizo yenu. Nyakati zijazo utakuja kukumbuka mazuri yake na kuona namna alivyokuwa anakutendea mambo sahihi kwenye uhusiano wenu. Ila mtihani mdogo tu ukakukimbiza.
Ni kweli ana dharau lakini anakupenda na wewe unampenda. Unatakiwa kuamini katika kufundisha, kwamba jukumu la kumuweka sawa lipo ndani yako. Haishindikani kutafuta muda ambao mambo yametulia halafu unamuelekeza kasoro zake za kukudharau ilhali mnapendana.
Mapenzi yanakuhimiza kuwa mvumilivu. Ana uhusika wako, vilevile wewe ni wewe, hamko sawa. Utakuwa unafanya kazi ya kutwanga maji kwenye kinu au kuchota maji bombani na kuyamwaga baharini kama utalazimisha awe na tabia ulizonazo.
Shika kanuni hii; ni kweli mwenzi wangu ana dharau, kutokana na tabia hiyo ananiumiza sana. Ila hiyo haiondoi ukweli kuwa tunapendana. Jukumu langu ni kumsahihisha mpaka akae sawa. Ni imani yangu kwamba nyakati zijazo ni za furaha na neema kwetu.
0 comments:
Post a Comment