Duru za uchunguzi zimeonyesha kuwa baadhi ya watu walioingia nchini kwa mwamvuli wa uchungaji wakitokea nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, majina yao yamo kwenye orodha ya wapiganaji wa kikundi hicho cha waasi.
Taarifa mbalimbali zilizokusanywa na gazeti hili zimeonyesha kuwa, raia hao wa Kongo mbali na kufanya kazi za kiroho, pia wanajihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na kufanya biashara ndogo ndogo.
Baadhi ya wachungaji waliozungumza Jumatano kuhusu suala hilo, walishindwa kukubali au kukanusha kuhusu taarifa hizo.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B, Assemblies of God, Getrude Lwakatare, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro (CCM), alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani iwapo anazo fununu za uwepo watu wa aina hiyo ambao kwa kiasi kikubwa wameanza kujenga taswira mbaya katika baadhi ya makanisa, alikaa kimya kwa muda kisha akakata simu.
Alipopigiwa tena na tena hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kuulizwa jambo hilo hakujibu.
Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Hokororo, yeye alipoulizwa kuhusu kuibuka kwa hofu hiyo na iwapo idara yake imekwishapata taarifa hizo alisema hazijamfikia.
"Taratibu za kupokea wageni kweli zinafahamika, lakini mpaka sasa hatujapata taarifa za uwepo wa watu wa aina hiyo. Lakini kama kweli wapo nchini, tunaomba tupatiwe taarifa kamili, wanasali wapi, lini na saa ngapi ili tufanye kazi yetu," alisema.
Aidha, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipotafutwa kuzungumzia taarifa hiyo naye alisema hana taarifa hizo.
Kamanda Kova alisema jambo hilo linaweza kuwa kweli, kutokana na mwingiliano mkubwa uliopo sasa wa raia wa kigeni nchini na alitoa wito wa kupatiwa taarifa za uhakika ili ziweze kufanyiwa kazi.
"Hilo suala ni la hatari sana na linatisha, naomba uzidi kunipa taarifa kwa kina ili tuanze kuchukua hatua za haraka, sikatai jambo hilo kuwepo kwa sababu ya mwingiliano uliopo sasa, lakini nawaomba wananchi kama walivyovuja taarifa kwenu, kwa sababu najua ninyi mko karibu sana na jamii, basi watusaidie na sisi hivyo hivyo tufanye kazi yetu," alisema Kova.
Kwa muda sasa, taarifa za kuwepo kwa watu wanaohofiwa kuwa wapiganaji wa kikundi cha waasi wa M23, waliojificha katika baadhi ya nyumba za ibada, zimezagaa jijini Dar es Salaam na baadhi ya makanisa ambayo wanaabudu yamekuwa yakitajwa.
Waasi wa kikundi cha M23, wanapigana vita na vikosi vya majeshi ya Serikali ya Kongo yanayosaidiwa na jeshi la Umoja wa Mataifa na hivi karibuni, ngome yao kuu ilisambaratishwa. Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment