Wednesday, 2 October 2013

KENYA ‘YAIKOMALIA’ MAREKANI

  

Westgate Mall kabla ya shambulio la magaidi
NAIROBI, Kenya
   Serikali ya Kenya imeilaumu Serikali ya Marekani kwa kuwaonya raia wake wasisafiri kwenda nchini humo kutokana na shambulizi la Septemba 21 mwaka huu, katika jengo la biashara la Westgate, jijini Nairobi, nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya, Bw. Joseph Ole Lenku, alitoa lawama hizo jana kwa waandishi wa habari wakati akizungumzia uchunguzi wa Serikali juu ya shambulizi hilo linalodaiwa kufanywa na wanamgambo wa Al Shabaab.
Bw. Lenku alisema kuwa, tahadhari hiyo kwa raia wa Marekani si ya kirafiki na Kenya ingawa uchunguzi huo, ulikuwa ukifanywa na polisi wa nchi hiyo, makachero wa Israel, Marekani na Ulaya.
Alipinga na kulaani ushauri wa Marekani kwa raia wake na kuwataka wathamini hali ya usalama wao binafsi kutokana na vitisho vya kigaidi vinavyoendelea na vya hivi karibuni katika Taifa hilo la Afrika Mashariki.
Ingawa hakuitaja moja kwa moja sekta ya utalii, maelezo ya Bw. Lenku yanaonekana kuhofia biashara hiyo nchini humo jinsi inavyoweza kuathirika katika kipindi hiki kwani sekta hiyo inaingiza dola za Marekani bilioni moja kila mwaka.
“Tumesikitishwa na ushauri huo ambao haukustahili, hauna umuhimu na si urafiki...unapingana na mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa,” alisema Bw. Lenku.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters la Uingereza, mbali na wahanga 50 wa Kenya, raia kutoka Uingereza, Ufaransa, China, Ghana, Canada, Australia, Afrika Kusini, Peru na Uholanzi pia waliuawa katika shambulizi hilo la kigaidi
Majira

0 comments:

Post a Comment