Wednesday, 2 October 2013

Chikawe afichua siri nzito muswada Katiba mpya

  

Ataja vifungu sita vilichomekwa
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
Serikali imekiri kuwa vifungu sita katika muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba vilivyoongezwa na kuwasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililopita, havikupelekwa Zanzibar kutolewa maoni.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE ofisini kwake iliyotaka kupata ufafanuzi kufuatia mfululizo wa malalamiko kuhusu muswada huo.

Muswada huo uliwasilishwa na kupitishwa na wabunge wa CCM na Augustine Mrema wa TLP katika mkutano wa 12 wa Bunge Agosti, mwaka huu na unasubiri uamuzi wa Rais wa kuusaini au la.


Chikawe alisema vifungu hivyo ambavyo havikupelekwa Zanzibar viliongezwa ndani ya Bunge na kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na kwamba haikuwa ajenda ya serikali.

Alisema vifungu vilivyoongezwa kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ambacho kiliwashirikisha wadau mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa ni suala la ongezeko la wajumbe watakaoshiriki Bunge maalum la Katiba kutoka 166 hadi 201.

Vingine ni Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu Baraza la Wawakilishi Zanzibar kusimamia mchakato wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba na Makamu wake pamoja na utaratibu wa kupitisha katiba kwa theluthi mbili kupitia kura ya maoni.

Chikawe alisema ndani ya Bunge yaliongezwa mapendekezo mengine matatu, ambayo ni ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wazo ambalo liliwasilishwa na Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM), sifa za Mwenyekiti wa Bunge la Katiba na ongezeko la idadi ya wajumbe watakaoteuliwa na Rais kutoka kwenye vikundi na taasisi kutoka watatu hadi tisa.

Alisema mapendekezo hayo sita yaliyoongezeka hayakupelekwa Zanzibar, lakini hilo halikuwa tatizo kwa sababu wabunge kutoka Zanzibar walishiriki kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar na wakakubaliana nayo na kuyapitisha.

“Kazi ya wabunge kutoka Zanzibar ni kuwakilisha maslahi ya Wazanzibari ndani ya Bunge, kwa hiyo pamoja na kwamba vifungu hivyo havikupelekwa Zanzibar siyo tatizo, wawakilishi wao ambao ni wabunge walikuwapo, na huo ndio utaratibu wa kupitisha/kutunga sheria,” alisema.

Alifafanua kuwa katika marekebisho ya awamu ya pili kabla muswada huo haujapelekwa bungeni, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walikutana na viongozi wa vyama vya siasa vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi na kujadili nini kiwamo kwenye mabadiliko hayo ya pili na wawakilishi wa vyama hivyo walitoa maoni.

Chikawe alisema serikali ilichukua maoni ya vyama hivyo na ikaandaa muswada huo na kuupeleka kwenye kikao cha Kamati ya Katiba na Sheria ya Baraza la Mawaziri na baadaye vifungu vilivyokuwa vimekubaliwa vikapelekwa Zanzibar.

Vifungu vilivyojadiliwa na kupelekwa Zanzibar ni jina la muswada uitweje, tafsiri ya neno Rasimu ya Katiba ni ipi na kanuni, mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge la Katiba ufanywe na Rais.
Vingine ni upatikanaji wa watumishi wa Bunge maalum la Katiba, utoaji wa maoni na muda wa Bunge hilo kukaa katika vikao uwe siku 70.

Aliongeza kuwa muswada huo kabla ya serikali kuupeleka Bungeni ulipelekwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Aboubakar Khamis Bakari, baada ya kukaa na viongozi wenzake walirejesha mapendekezo yao Mei 31, mwaka huu.

Katika mapendekezo ya SMZ, walisema suala la uteuzi wa wajumbe 166 wa Bunge la Katiba ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, muda wa Bunge hilo uwe siku 90 badala ya 70 na suala la uwiano wa jinsia kwa wajumbe.

Alisema baada ya kupata mapendekezo hayo kutoka SMZ, serikali ikayaingiza kwenye muswada huo baadaye Spika aliupeleka kwa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na kabla ya kusomwa bungeni, kamati hiyo iliwaita tena wadau vikiwamo vyama vya siasa kutoa maoni yao.

UKOMO WA TUME YA JAJI WARIOBA
Chikawe alisema suala hilo lilipendekezwa na Mbunge wa Kisarawe, Jafo ambaye alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapowasilisha ripoti yake ivunjwe sababu haitakuwa na kazi na kama Bunge la Katiba litahitaji ufafanuzi wowote ataitwa Mwenyekiti wa Tume hiyo kufafanua.

Kuhusu suala la wajumbe wa kuteuliwa Zanzibar kuwa 55 tu kati ya 166, alisema hilo liliamuliwa kwa sababu uwakilishi wenyewe ni wa kupiga kura, hivyo uwingi wa watu nao ulizingatiwa kwani Zanzibar ni wachache wakati Tanzania Bara ni wengi.

MUSWADA KUHODHIWA NA CCM
Chikawe alisema kama unachukua Bunge kwa misingi ya chama siyo sawa, lakini bunge halikukutana na kupitisha muswada huo kwa misingi hiyo.

“Kitu cha msingi ni kwamba quorum (akidi) ya wabunge ilitimia wakati wa kupitisha muswada huo, hivyo sheria haikuvunjwa, sikuona sababu ya wabunge wa upinzani kutoka bungeni,” alisema.

KUMTISHA RAIS ASIPOSAINI MUSWADA
Alisema yeye (Chikawe) hana ubavu wa kumtisha Rais kwani Rais ana hiari ya kuusaini muswada huo au kutousaini na kwamba ana imani atausaini.

Vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema vimeshaungana kuupinga muswada huo kwamba utaleta katiba mbaya kutokana na mchakato mzima kuhodhiwa na CCM.

Wenyeviti wa vyama hivyo, Profesa Lipumba (CUF), Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Mbowe (Chadema) wamekwisha kufanya mikutano miwili ya hadhara jijini Dar es Salaam na Zanzibar kwa lengo la kuwashawishi wananchi waupinge mchakato wa katiba.

Kuvunjwa kwa Tume kabla ya kura ya maoni pia ni moja ya hoja zinazotumiwa na upinzani kupinga mchakato wa katiba kwa maelezo kuwa hatua hiyo itasababisha kutokuwapo na mjumbe halali wa Tume wa kwenda kutoa maelezo katika bunge la katiba ikiwa watahitajika kwa kuwa watakuwa wameshapoteza uhalali wa kuwa wajumbe.

Pia muungano huo unapinga muswada huo kwa kuwa haukuzingatia maoni ya Zanzibar kwa kuwa hawakushirikishwa kabla ya kuwasilishwa bungeni

Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba wiki iliyopita alizungumza na waandishi wa habari na miongoni mwa kauli zake ni mshangao wake juu ya pendekezo la kuvunjwa kwa Tume hiyo kabla ya kumalizika kwa kura ya maoni. Alisema wazi kuwa muswada huo unavunja sheria mama, yaani sheria ya Marekebisho ya Katiba.

 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment