Wednesday, 2 October 2013

WATANZANIA HAWAAMINIKI KIMATAIFA, WADAIWA KUPENDA 'MICHONGO'...

  

Balozi Ombeni Sefue.
Kuporomoka kwa maadili ya Mtanzania, kumetajwa kuporomosha hadhi ya Mtanzania ndani na nje ya nchi, na sasa wawekezaji wanaogopa kuwaajiri.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wadau mbalimbali katika kuinua kiwango cha uwajibikaji na maadili katika utumishi wa Umma, mafunzo yaliyoandaliwa na Sekretarieti ya  Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mbali na raia na viongozi kukosa maadili, imeelezwa kuwa hata vyombo vya usalama vinavyoaminiwa, vimepoteza maadili kiasi cha kusababisha raia wema kuogopa kutoa ushirikiano kwao.
Akielezea hadhi ya sasa ya Mtanzania kimataifa, Balozi   Sefue alisema mmomonyoko huo wa maadili umesababisha hata pasi za kusafiria za kitanzania kutiliwa mashaka na Watanzania wote kuonekana kama watenda maovu, huku akigusia biashara ya dawa za kulevya inavyochafua nchi.
"Zamani pasi za kusafiri za Tanzania ili kuwa kama bendera, ilisaidia sana kufungua milango ya biashara na uwekezaji, lakini hivi leo pasi hizo zinatiliwa mashaka na Watanzania wote wanaonekana ni waovu," alisema Balozi Sefue.
Alisema mmomonyoko huo pia upo kwa baadhi ya viongozi na hata wananchi wa kawaida, na umewafanya wawekezaji kuanza kuogopa kuajiri Watanzania kwenye baadhi ya nafasi za ajira.
"Wapo wawekezaji wa ndani na wa nje nimezungumza nao na wao wana wasiwasi, wanaogopa Watanzania na hata wanashindwa kuwaajiri kwenye baadhi ya nafasi kwa kile wanachosema, Watanzania hawana maadili na wanapenda 'michongo', sasa hii ni mbaya kwa sifa ya nchi yetu," alisema Balozi Sefue.
Alisema si jambo baya Watanzania kuwa na mali, lakini ni vyema mali walizonazo zifahamike walivyozipata kwa njia halali au lah.
"Hatusemi kuwa na mali ni vibaya hapana, lakini tunataka utuambie mali ulizojilimbikizia kama umezipata kwa njia halali, kwa maana wapo wasio waadilifu waliopata mali kwa njia zisizo halali," alisema Balozi Sefue.
Katibu wa Viongozi wa Siasa wa Sekretarieti hiyo, Laura Maro,    alisema mmomonyoko wa maadili haupo tu kwa baadhi ya viongozi wa umma na wananchi, bali pia kwa vyombo vya usalama ambavyo vinaaminiwa.
Alisema wakati mwingine vyombo hivyo vinakosa maadili kwa kutaja majina ya raia wema wanaotoa taarifa za wahalifu au wafanyabiashara haramu, jambo linalowafanya raia kuogopa usalama wao na kutotaja tena wahalifu.
"Maadili yameporomoka sio kwa viongozi au wananchi pekee, bali hata kwa vyombo vya usalama ambavyo vinaaminiwa, wakati mwingine vinakosa uadilifu sasa tunataka maadili yarudi ili kuijenga nchi yetu," alisema Maro.
Balozi Sefue alikiri sio wote ni waadilifu ndani na nje ya Serikali, hivyo mapambano ya kurejesha uadilifu lazima yafanywe kwa ushirikiano na wadau wote, ili kurejesha maadili nchini.
Alisema suala la kurejesha maadili si kazi nyepesi, bali ni jambo linalohitaji ushirikiano kuanzia ngazi ya familia kwa watoto na wazazi kuelekezana jinsi ya kuboresha maadili na pia kwa viongozi na watumishi wa umma.
Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti hiyo, Jaji Salome Kaganda, alisema warsha hiyo itajenga ushirikiano na wadau mbalimbali katika jamii, ili kupokea maoni na mapendekezo ya namna ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili nchini.

0 comments:

Post a Comment