Mganga akamatwa na hirizi zenye chura
wanaopumua akizitumia kuwauzia wahamiaji haramu wasiweze kukamatwa
katika Operesheni Kimbunga
Na Mwandishi Wetu, Kibondo
Kampeni ya kitaifa ya kuwaondoa wahamiaji haramu nchini iliyopewa jina
la “Operesheni Kimbunga”, imezidi kuibua mambo mazito baada ya mganga wa
kienyeji, kugundulika akitumia uchawi ili kuwalinda wahamiaji hao
wasikamatwe
. Mganga huyo aliyefahamika kwa jina la Bw. Bahalaye Gwenda (60), ameifanya kazi hiyo tangu kuanza kwa operesheni hiyo kwa kuwalipisha wahamiaji haramu sh. 200,000 kila mmoja wasiweze
. Mganga huyo aliyefahamika kwa jina la Bw. Bahalaye Gwenda (60), ameifanya kazi hiyo tangu kuanza kwa operesheni hiyo kwa kuwalipisha wahamiaji haramu sh. 200,000 kila mmoja wasiweze
kukamatwa na vyombo vya dola vinavyofanya kazi hiyo.
Tukio
hilo la kustaajabisha, limetokea katika eneo la Kigaga, Wilaya ya
Kibondo, mkoani Kigoma ambapo mganga huyo hutumia hirizi ambazo ndani
yake kuna dawa za kienyeji na vyura wanaopumua kuwauzia wahamiaji hao.
Taarifa
za mganga huyo, ziliifikia Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo
ambapo Mwenyekiti wa kamati hiyo Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Venance
Mwamotto, aliongoza kikosi kazi cha wajumbe wa kamati, polisi hadi
nyumbani kwa mganga.
Kamati
hiyo ilipata malalamiko hayo kutoka kwa wahamiaji ambao walikamatwa
mbali ya kupewa dawa na mganga huyo ambaye ni raia wa nchi jirani ya
Burundi.
Mazingira
ya kamati kufika nyumbani kwa mganga huyo yalikuwa kama sinema ambapo
wajumbe wa kamati wakiwa na askari polisi, baada ya kukaribia nyumba
yake mganga akiwa ameshika mzizi mkononi na kibuyu kilichofungwa hirizi,
aliwapa ishara ya kutosogelea nyumba hiyo.
“Wakati
tukiwa mbele yake tukimfuata, alituambia tusisogelee nyumba yake kwani
uchawi alionao una nguvu kubwa hivyo unaweza kutudhuru, hatukumsikiliza
tuliendelea kumfuata hivyo alitupa vifaa vyake chini na kukimbilia
ndani.
“Baadhi yetu walikuwa waoga katika
eneo husika wakiogopa kudhurika, alipoingia ndani, alitokea mlango wa
nyuma na kukimbia na sisi baada ya kuingia ndani, tulichukua vifaa vyake
kama ushahidi,” alisema Bw. Mwamotto.
Aliongeza
kuwa, kikosi kazi alichokiongoza kiliamua kwenda nyumbani kwa mganga
huyo kwa lengo la kumkamata kutokana na malalamiko waliyopata kutoka kwa
wateja wake ambao walidai kutumia fedha nyingi kumpa mtaalamu huyo
hivyo walitaka kurudishiwa fedha zao.
Alisema
baada ya kuzipasua hirizi walizozikuta, vibuyu na pembe, walikuta dawa
za kienyeji pamoja na chura wazima wanaopumua. Vitu vingine
walivyovikuta ni vitambaa vyeusi, vyeupe, vyekundu na vitu vingine vya
ajabu.
Akizungumzia operesheni hiyo wilayani humo, alisema wamefanikiwa
kukamata sare za Jeshi la Burundi na kofia vilivyokuwa vikitumika katika
matukio mbalimbali ya uhalifu na wahamiaji haramu.“Tunaendelea
na operesheni yetu kwa kushirikiana na viongozi ili kuhakikisha
wahamiaji wote haramu wanarejeshwa nchini mwao tuweze kurudisha amani na
usalama,” alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama Mkoa, Issa Machibya, alisema wahamiaji haramu wengi walikuwa
wakijihusisha na matukio ya ujangili na biashara ya silaha zikiwemo za
kivita.
Alisema Mkoa huo pekee umewakamata wahamiaji haramu 4,365 kutoka nchini
Burundi katika awamu ya kwanza ya operesheni iliyosambaa katika mikoa
mbalimbali nchini na kuwataka wakazi wa Kigoma, kushiriki kikamilifu
katika vita hiyo.
Kwa mujibu wa kiongozi wa timu ya Habari na Mawasiliano ya Operesheni
Kimbunga, Zamaradi Kawawa, alisema katika operesheni hiyo awamu ya pili
iliyofanyika Mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera, bunduki moja aina ya SMG,
bastola moja, magobole 17 na risasi 115 zikiwemo za bunduki aina ya SMG
102 na 13 za bastola vilikamatwa.
Wahamiaji haramu waliokamatwa wengi wao ni kutoka nchi za Burundi
ambapo raia wake 114 walikamatwa wakiishi nchini kinyume na sheria na
raia 20 wa Rwanda ambao nao walikamatwa katika kipindi hicho
Majira
0 comments:
Post a Comment