Kuna wakati unaona maisha yako hayana maana au umechoshwa na
maisha, hivi ndivyo tulivyo licha ya kuwa maisha ni yaleyale. Kwa bahati
nzuri tunawezabadilika kwa jinsi tunavyoona maisha yetu yalivyo na kwa namna tunavyotaka
yawe. Ulishawahi kusikia watu wakisema “maisha yapo tu, ni wewe mwenyewe na
maisha yako.’’
Furaha
hutegemea sana wewe mwenyewe kuliko vichocheo vingine vya
nje vya kimazingira. Ninamaana licha ya kuwa unaona maisha ni magumu
huna sababu ya kucheka au kufurahi lakini hizo zote ni sababu unazoziona
wewe mwenyewe, ningependa kukuona leo mwenye matumaini na faraja na
maisha yako. Huna sababu ya kununa au kuwa mnyonge kwasababu hata ukiwa
huna furaha hutatua chochote, ni heri kuwa na matumaini na maisha yako
na kutafuta ufumbuzi wa matatizo uliyonayo kwani hiyo ndiyo njia ya
kuondekana na maswahibu uliyonayo.
Haya ni
mambo kadhaa ambayo yatakusaidia kuwa mwenye furaha na maisha yako licha
ya maudhi unayopata kwa watu tunaoishi na kufanya nao mambo mbalimbali
ya kila siku.
1. Samehe watu waliokukosea.
-Jua ya
kwamba hakuna mtu aliyekamilika, mtu anaweza kukufanyia
kitu kibaya ama kwa makusudi au bahati mbaya lakini yote atakuwa
amekukosea.
Kukaa au kuishi na kisirani kwasababu ya mtu au watu waliokufanyia ubaya
kwa
muda mrefu kutakuletea matatizo ya kiafya ( depression ) au kuharibu
kabisa uhusiano wako na watu uliogombana nao. Kuwa msahaulifu wa maudhi
unayopata kwa watu, waelewe na ikiwezekana waepuke lakini usiwe na
kisirani nao.
2. Kuwa mkarimu kwa watu wote.
-Ukiwa mkarimu kuna baadhi ya watu watakusema vibaya ili
mradi tu watu wengine wakuone mbaya, mchoyo au mtu wa kujigamba. Ni vyema ujue
sio wote watakaona wema wako, hivyo usitegemee shukrani sana. Kuna msemo wa
kiswahili ‘’unasema tenda wema na uende zako’’ nina maana ya usitegemee ahsante
kupita kiasi kutoka kwa watu. Hii itakusaidia kutojali na kuumia sana
pale utakapoona watu hawajachukulia mchango wako kwa uzito ulioutegmea.
3. Chagua kuwa mshindi wa maisha yako.
-Mafanikio
yako yanaweza kuvutia watu, utakapo pata
mafanikio jua kwamba utapata marafiki wazuri, wasio wa kweli na maadui
wachache. Endelea kuwa mshindi na siku zote chagua kufanya mambo yako
kwa uhodari na kuamini utaendelea kufanikiwa licha ya watu kukuvunja
moyo au kudharau unachofanya. Kumbuka kila mtu anatamani mafanikio ila
wachache kama wewe mwenye kujibidiisha ndio washindi hivyo tegemea
kupata watu wasiokupenda kwani ''mti wenye matunda haukosi kupigwa mawe.''
4. Kuwa mtu mkweli na muadilifu.
-Hakuna
mtu anayependa kudanganywa, kutapeliwa, kutendwa vibaya kwa namna
yeyote ile sidhani hata wewe binafsi kama utapenda ufanyiwe hivyo.
Malipo ya uadilifu ni watu kukuamini na kukutegemea katika mambo
mbalimbali ya kijamii, kikazi au hata kisiasa, watu watakupenda kwa kuwa
unaaminika kwa utashi na umahiri wako hivyo wanaweza kukupatia kazi,
kukuomba uwaongoze kwa kukupatia cheo kikubwa nakadhalika. Vizuri zaidi
hata familia yako nao watakupenda na kuiga mfano wako.
5. Jenga maisha yako kwa kadri uwezavyo.
-Ulichojenga
leo kwa muda wa miaka mingi kinaweza bomolewa kwa siku moja na mtu
mwingine. Hata hivyo huna sababu kutojenga maisha yako kwasababu ya
kuogopa watu wengine, fanya uwezalo kama ni kuboresha nyumba unayoishi,
afya yako au kazi inayokupatia kipato kila siku. Usichukulie maisha
katika upande mbaya kwa kusema ''hata nikitafuta mali nitaziacha hapahapa duniani'' hiyo
ni dhana mbaya kwasababu hata hao waliotengeneza magari tunayotumia leo
kusafiria, wataalamu wa afya wanaotutibu tunapoumwa, wakandarasi
wanaojenga majengo tunayotumia kama ofisi kwa kazi mbalimbali laiti nao
wasingefanya kazi zao basi leo tusingeweza kurahisisha maisha kama
tunavotumia matunda ya kazi zao.
6. Fanya mambo mazuri kwa maslahi yako na ya watu wengine.
-Utafanya
mazuri lakini baadhi ya watu hawatatosheka na msaada wako, hakuna haja
ya kuwajali sana watu wa aina hiyo maana hawataweza kurudhika kwa
chochote utakachowafanyia kiwe kidogo au kikubwa. Saidia kufanya mambo
mbalimbali ya kimaendeleo katika mji wako kwani hiyo ndiyo namna ya
kuonyesha uungwana wako kwao. Usisahau vilevile kufanya kwako mambo ya
msingi katika jamii ndio mwanzo wa kupata mengi kwa watu unaowasaidia.
7. Jishirikishe na kujitolea kusaidia wengine kwa namna
yeyote ile.
-Shirikiana
kwa hali na mali na watu wengine, huwezi kuishi mwenyewe hata kama una
pesa, mali, chakula na kila kitu unachodhani ukiwanacho utakaa mbali na
walimwengu. Dunia ya sasa inajengwa kwa kushirikiana hivyo ukitaka
kufanikiwa na maisha yako penda kushirikiana na wenzako na kila kitu
utapata kutoka kwa kwao. ''You receive more by giving more.'' amini
kila kitu unachotaka kipo kwa watu wengine, ni wewe tu kuwa nao pamoja
na kujenga umoja. Huwezi kuwa na kila kitu ila unawezapata vitu utakavyo
kwa watu wengine.
WORD OF THE DAY: ''Happiness is by ch0ice, not by chance.''
Kama una chochote cha kuongeza kuhusiana na mada hapo juu,
tafadhali usisite kutoa maoni yako!
0 comments:
Post a Comment