Kuna aina nyingi sana za tabia mbaya, lakini bila shaka zile kubwa kabisa ziko sita. Hii ina maana kwamba mtu anapoishi popote ajue kwamba, kwa njia moja au nyingine atakuwa anapambana na watu wa tabia hizi:
1. Kuna wale watu ambao ni wakali na wenye hasira sana, ambao mambo yao ni kama ya kulazimisha tu. Watu hawa hawana simile, kwani wanaweza kufanya jambo kubwa , baya au la hatari na baadaye ndiyo wakaanza kufikiri. Kwa kawaida , watu hawa wanaamini kwamba, kwa kuwa mkali na kuonyesha hasira na ubabe, ndipo mtu anapoweza kufanikiwa katika jambo.
2. Kuna lile kundi la watu ambao, wao kazi yao ni kulalamika tu. Kila siku wanalalamika kuhusu mambo au vitu wasivyovipenda au kuvitaka kwenye maisha yao. Lakini, watu hawa kamwe huwa hawachukui hatua za kubadili hali. Mtu analalamika kuhusu kazi yake, lakini kutafuta nyingine au kuiacha hawezi au hayuko tayari. Wenye tabia hii wapo wengi sana hapa JF.
3. Kuna lile kundi la watu ambao wenyewe ni watu wakimya kabisa. Ni watu ambao kila utakachowaambia au kuwaomba watakuwa wakiitika tu ‘ndiyo.’ Wenyewe huwa hawajui kabisa neno linaloitwa ‘hapana.’ Lakini ni watu ambao kamwe hawafanyi kile walichokubali kwamba, watakifanya. Kwa hiyo, hawakatai , lakini hawatendi walichokubali kukitenda. Hapa naogopa kuwataja baadhi ya watu humu JF wenye tabia hii…..
4. Kuna kundi la watu ambao tunaweza kuwaita kuwa ni watu wa ‘hapana.’ Hawa ni watu ambao hata ubuni kitu gani watakwambia tu, kwamba hicho hakiwezekani au hakina maana. Ni watu ambao wanaamini kwamba, ni wao peke yao tu wanaomudu kufanya mambo au wenye uwezo mkubwa wa kujua au kufanya.hawa ni wagumu sana katika kumpa mtu moyo wa kumudu jambo.
5. Kuna wale ambao nao kidogo ni kama hao hapo juu. Hawa huamini kwamba, wanajua kila kitu, wao ndiyo wenye njia bora ya kutatua tatizo, za kufikia muafaka na kurekebisha tatizo. Hata kama hawana utaalamu kabisa na kitu, lakini watawaonyesha wataalamu kwamba, waondio wanaojua zaidi kuhusu kitu hicho.ndipo pale unapoona mwenye nyumba anabishana na mjenzi na mjenzi anapofuata maelekezo ya mwenye nyumba , hatimaye nyumba huporomoka baada ya muda mfupi.
6. Kuna wale watu ambao wenyewe hawawezi kufanya jambo likakamilika. Ni hadi watu wengine waingilie na kulifanya kwa sababu ya kuona linachelewa au limesimama. Inaweza ikawa ni kazi ya ofisini , nyumbani au kwingine. Hawa huahirisha kufanya jambo hadi inakifu. Kila siku wao wanasema watamaliza baadaye au kesho au sasa hivi, lakini hawamalizi wanaahirisha tu………
boss ngassa blog
0 comments:
Post a Comment