Saturday, 24 August 2013

JWTZ LAFANYA MSAKO MKALI WA OFISA WAKE ALIYETOROKA MIEZI MINANE ILIYOPITA...

Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) linamtafuta popote alipo ndani na nje ya nchi ofisa wake, Luteni Kanali Celestine Seromba aliyetoroka jeshi zaidi ya miezi minane sasa.

Msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba alisema jeshi hilo, halijajua ofisa huyo katorokea wapi, lakini halitapumzika kumsaka mpaka watakapompata popote pale alipo.
Meja Komba alisema hayo wakati akitoa tamko la jeshi na ufafanuzi kwa waandishi wa habari jana, kufuatia habari zilizoandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari vya nje na ndani, ambavyo viliripoti kutoroka kwa Luteni Kanali Seromba.
“Ni kweli Ofisa mtajwa alikuwa Ofisa wa JWTZ na alikuwa akikabiliwa na makosa ya kijeshi, huenda hiyo ndio sababu ya kutoroka kwake. Jeshini utoro ni kosa ambalo haliwezi kufutika, hivyo ofisa huyu anaendelea kutafutwa na akipatikana hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.
Meja Komba alisema mtu huyo alisimamishwa kwa makosa ya kijeshi, ambapo jeshi lilishaanza uchunguzi kufuatia makosa hayo na kwamba alitoroka usiku wa Desemba 17 kuamkia Desemba 18, mwaka 2012.
Msemaji huyo wa jeshi alikanusha ofisa huyo kutoroka na nyaraka za jeshi hilo na kuongeza kuwa jeshi lilipoanza kuchunguza tuhuma dhidi yake alikabidhi kila kitu alichokuwa akitumia kufanyia kazi zake kama mkufunzi wa masuala ya kompyuta.
Alikanusha ofisa huyo kuwa Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Mawasiliano (IT) wa jeshi hilo, bali alikuwa mkufunzi wa kawaida wa masuala ya kompyuta na kumtaja Mkuu wa Kitengo hicho kuwa ni Kanali Obeid.
Kwa mujibu wa Meja Komba, kutokana na nafasi aliyokuwa nayo ya ukufunzi, taarifa zilizokuwa nikipita mikononi mwake ni masuala ya wanafunzi na hakuna taarifa yotote nyeti, iliyokuwa ikimfikia na kuongeza kuwa labda uzoefu wake aliopata wa masuala ya kompyuta, ndio anaweza akatumia huko alipo.
Akifafanua kuhusu uraia wa ofisa huyo alisema, Luteni Kanali Seromba ni Mtanzania aliyezaliwa Rukila mkoani Kagera na kwamba alisoma katika Shule ya Msingi Rukila, kisha alijiunga na Shule ya Sekondari Lulenge na Kidato cha Tano na Sita alisoma katika Shule ya Sekondari Minaki.
Meja Komba alisisitiza kuwa, “ Luteni Kanali Seromba ni Mtanzania, hajatoroka na nyaraka zozote za kijeshi na jeshi linaendelea kumtafuta ofisa huyo na akipatikana atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria”. Aliahidi kuwa jeshi litaendelea kuwapa wananchi taarifa kila mara kuhusiana na suala hilo.
Awali, baadhi ya vyombo vya habari, viliripoti kuwa ofisa wa cheo cha juu wa jeshi hilo, ambaye anadaiwa kuwa na asili ya Rwanda, ametoweka katika mazingira ya kutatanisha huku akidaiwa pia kuondoka na nyaraka nyeti za jeshi hilo.

0 comments:

Post a Comment