Patashika katika jengo la Westgate Shopping Mall mjini Nairobi. |
Wakati Serikali ya Kenya
ikitangaza kukamilisha kazi ya kupambana na magaidi walioteka kituo cha
biashara cha Westgate, Nairobi na kufanikiwa kuwaangamiza, mfanyakazi wa
moja ya maduka ya kituo hicho, amesema mwanamke anayefanana na Samantha
Lewthwaite alimmiminia risasi siku ya tukio.
Shuhuda huyo alisema alikutana uso kwa uso na mwanamke mwenye rangi nyeupe na nywele ndefu nyeusi akiwa na bunduki aina ya AK-47– kama Mwingereza Mwislamu anayetuhumiwa kutoa mafunzo kwa magaidi, Lewthwaite- wakati amejificha karibu na kasha ndipo akammiminia risasi.
Katika hali ya kushangaza, mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Caroline, hakudhurika na risasi hizo wakati magaidi hao wakivamia duka hilo Jumamosi.
Alisema: “Alikuwa juu kidogo lakini si mbali na mimi, alikuwa karibu, kiasi kwamba niliweza kumwona akiangaliaangalia sakafuni nilikokuwa hatimaye akaniona. Alisimama na kunilenga na kufyatua bunduki. Risasi zote hazikunipata, sijui nini kilitokea!
“Ghafla aliacha kunishambulia kwa muda na kuangalia pembeni na niliruka na kukimbilia kwenye kona na ndivyo nilivyoweza kutoroka. Alikuwa na ngozi nyeupe na nywele ndefu nyeusi na alivaa baibui jeusi. Sikumbuki vizuri, lakini nakumbuka alikuwa mweupe.”
Ofisa wa kupambana na ugaidi wa Kenya juzi usiku alibainisha kwamba polisi wamepokea ushahidi mwingi wa mwanamke miongoni mwa magaidi hao anayefanana na mjane wa Jermaine Lindsay anayetuhumiwa kwa ugaidi wa kujitoa mhanga.
Aliongeza: “Tunaamini kwamba alihusika na shambulio hilo. Hatuna shaka na mashahidi walioshuhudia ambao wanasema walimwona akiongoza na kutoa maagizo kwa washambuliaji.”
Maelezo ya jinsi alivyo mwanamke huyo yalithibitishwa na kauli ya Rais Uhuru Kenyatta juzi usiku, kwamba alipokea taarifa za kiintelijensia zikisema kuwa kuna mwanamke Mwingereza ambaye alihusika katika shambulizi hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed naye aliongeza: “Mwingereza huyo alikuwa mwanamke…alishafanya matukio haya mara nyingi.”
Juzi, taarifa kwenye Twitter ya kikundi cha al Shabaab ilidai kuwa Lewthwaite ndiye alikuwa akiamuru magaidi kushambulia.
Maofisa usalama wa Uingereza walisema bado hawajapokea uthibitisho wowote kutoka Kenya kuhusu uhusika wa Lewthwaite katika shambulizi hilo, lakini wakasema hawatashangaa wakisikia amehusika.
Ilisemekana pia juzi kwamba bibi wa Lewthwaite, Ellen Allen (85) alikimbizwa hospitalini Banbridge, Ireland Kaskazini, baada ya kuzimia kutokana na msongo wa mawazo uliosababishwa na utukutu wa mjukuu wake huyo.
Lewthwaite amekuwa akitafutwa tangu Polisi ilipozima njama zake za kulipua bomu Mombasa, Kenya mwaka 2011, juzi kesi dhidi ya mwenzake, Jermaine Grant ilianza mjini humo.
Maofisa wa kupambana na ugaidi wa Uingereza -Scotland Yard-walitoa ushahidi wao katika kesi hiyo wakizungumzia kemikali zilizokutwa katika kiwanda chao kidogo cha kutengeneza mabomu.
Noel Hogan, ambaye alimhoji mwanafunzi huyo wa zamani wa sarufi muda mfupi kabla ya milipuko ya mabomu ya Julai 7, alisema: ”Kama Samantha anahusika, hainishangazi.”
Hogan alikodiwa na benki kuchunguza kwa nini mteja wao, mume wa Lewthwaite, Lindsay, alitumia pauni 900 kununua chupa kadhaa za marashi kwa siku chache.
Ununuzi huo unaotia shaka, ulifanyika siku chache kabla ya shambulizi hilo la Julai 7 na marashi hayo yalitumika kutengenezea milipuko nyumbani.
Waliomfahamu Lewthwaite tangu udogo nyumbani kwao Aylesbury, walieleza kushangazwa na yeye kuhusika kama mmoja wa wafadhili wa al Shabaab na mkufunzi wa utengenezaji mabomu.
Diwani Raj Khan alisema: “Alikuwa msichana kijana Mwingereza wa kawaida tu. Hakuwa anajiamini sana. Sikuwa na chochote cha kumshuku.” Lewthwaite alikuwa mjamzito wa miezi saba wakati mumewe alipojilipua na kuua watu 26.
Wakati magaidi wamepagawa wakifyatua risasi ovyo, pengine mama na wanawe wawili hisia zao zingewasukuma kukimbia na kuokoa maisha yao. Lakini familia hiyo iliepuka mauaji hayo kwa kufikiria haraka na kujifanya wamekufa ili wanusurike.
Mama na wanawe wawili walilala chini na ‘kujikausha’ huku akiwa amewawekea mkono wake mgongoni wanawe hao.
Ni kutokana na utulivu waliokuwa nao katika mazingira hayo ya kutisha, ndipo polisi mmoja alipotambaa na kupata nafasi ya kuwaokoa.
Kelele za magaidi zilisikika kwa nyuma yao, na hicho ndicho pengine kilionekana kuwashawishi kuinuka na kukimbia.
Ofisa wa Polisi alimchukua msichana mkubwa na mdogo na kukimbilia nje mama akifuatia. Msichana mkubwa aliendelea kushikilia mfuko wa vitu walivyokuwa tayari wamenunua dukani hapo.
Licha ya Rais Kenyatta kutangaza ushindi wa majeshi yake, al Shabaab ilidai jana kuwa mateka 137 waliotekwa nao dukani hapo walikufa.
Hata hivyo, maofisa wa Serikali hawakuthibitisha idadi hiyo, ambayo iko juu kuliko iliyotangazwa na Serikali kuwa ya watu waliopotea na kuzidi pia 72 ambao ndiyo wanaodaiwa kupoteza maisha wakiwamo wapiganaji watano kama ilivyotangazwa na Rais juzi.
Wapiganaji wa al Shabaab katika ujumbe wao kupitia Twitter walisema mateka 137 waliokuwa wakishikiliwa na mujahidina walikufa na kuelekeza lawama kwa Serikali ya Kenya.
Katika ujumbe mwingine, wapiganaji hao pia wanalaumu vikosi vya Kenya kwa kutumia kemikali kumaliza sintofahamu hiyo ya siku nne, kabla ya ‘kubomoa’ duka hilo.
“Katika kitendo kinachoonekana cha uoga, vikosi vya Kenya vilivyokata tamaa viliamua kwa makusudi kutumia kemikali…na katika kuficha uhalifu wao, Serikali iliamua kuvunja jengo hilo na kufukia ushahidi na mateka wote wako chini ya kifusi.”
Hata hivyo msemaji wa Serikali Manoah Esipisu mara moja alikanusha madai hayo na kusisitiza hakuna silaha za kemikali zilizotumika na kwamba idadi ya raia waliouawa ni 61.
“Al Shabaab inajulikana kwa madai potofu na hakuna ukweli wowote katika wanachokisema,” alisema.
Esipisu alisema sakafu za duka hilo zilibomoka baada ya mashambulizi kuanza na kusababisha udhaifu katika sakafu hizo na ya juu kuangukia ya tatu ambayo ni eneo la maegesho na kuangulia ya pili hadi ya kwanza na ya chini.
Juzi usiku wakati Rais Kenyatta alihutubia Taifa, milio ya bunduki iliendelea kusikika, ambapo Esipisu alisema ilitoka kwa vikosi vya Kenya vilivyokuwa vikipekua chumba hadi chumba katika duka hilo, vikifyatua risasi kujihami kwani havikuwa vikijua ndani kuna hatari gani.
Alisema: “Wakati wa safishasafisha unapokuwa umedhibiti eneo unapoingia chumbani ambako hujaingia kabla unapaswa kufyatua risasi kuhakikisha kwamba hauingii mtegoni. Hakukuwa na majibizano kutoka kwa magaidi kwa zaidi ya saa 36.”
Wakati huo huo, Serikali ya Kenya ilitangaza kwamba wataalamu kutoka Uingereza, Marekani na Israeli watasaidia uchunguzi juu ya shambulizi hilo. “Kituo hicho kimefungwa kwa sababu ni eneo la uhalifu,” alisema Esipisu.
Jana mchakato wa kuondoa miili katika duka hilo haukuwa umeanza, pengine kutokana na hali kwamba haijawa salama sana, ingawa maofisa wa mochari ya Jiji la Nairobi walisema wafanyakazi wao wanajiandaa kwenda katika jengo hilo.
Kulikuwa pia na hofu kwamba baadhi ya magaidi wanaweza kuwa bado wako hai katika kifusi ndani ya jengo hilo lenye maduka mengi ya rejareja kama vile ya bidhaa za Bose, Nike na Adidas, benki, migahawa na casino.
Ofisa mwandanizi wa usalama anayehusika na uchunguzi alisema itachukua muda mrefu kupekua jengo lote kabla ya kutangaza rasmi kuwa tishio la magaidi halipo tena. Siku tatu za maombolezo kitaifa zilianza jana.
Al Shabaab, ambayo inamaanisha kijana kwa Kiarabu, ilianza kutishia Kenya na shambulizi la kigaidi mwaka 2011, baada ya Kenya kupeleka vikosi vyake Somalia baada ya kutokea utekaji nyara wa raia wa mataifa ya Magharibi ndani ya Kenya.
0 comments:
Post a Comment