Cheka anatarajia kusoma masomo ya Kiingereza na Biashara.
Dar es Salaam. Leo
bingwa wa dunia wa WBF, Francis ‘SMG’ Cheka ataandika historia mpya ya
maisha yake kwa kuanza rasmi masomo yake ya awali ya sekondari katika
shule ya St Joseph mjini Morogoro.
Cheka anayepigania uzani wa super middle (kg 76) alifikia uamuzi wa
kurudi shule baada ya kupewa ufadhili na Shule ya Sekondali ya St
Joseph.
“Sijui masomo yatakuwaje, lakini vyovyote itakavyokuwa nitapambana nayo
kwani uamuzi wa kurudi shule umetoka moyoni hivyo sitateteleka, lakini
kabla ya kwenda shule nitaanza mazoezi kwanza,” alisema Cheka katika
mahojiano na Mwananchi.
Cheka baba wa watoto wawili, Boniface na Historia anadai alikuwa na
ndoto za kujiendeleza kielimu tangu zamani japo alishindwa kutokana na
majukumu ya kifamilia.
“Naenda kusoma kweli, sitafanya mzaha hata kidogo kwenye masomo yangu,
pia sitaacha kufanya mazoezi kwani Desemba natakiwa kutetea taji langu
la dunia,” alisema bondia huyo asiyekamatika hapa nchini kwenye ngumi za
kulipwa.
Cheka alihitimu elimu yake ya msingi miaka kadhaa iliyopita Shule ya
Msingi Kinondoni B, Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa bondia huyo
hakubahatika kuendelea kutokana na matatizo ya kifamilia na kujikita
kwenye ngumi za ridhaa wakati huo kabla ya mwaka 2000 kujiunga rasmi
kwenye ngumi za kulipwa.
Tangu wakati huo amefanikiwa kutwaa ubingwa wa taifa, mataji ya Afrika
ya UBO, IBO, IBF, WBC na WBO kabla ya mwishoni mwa Agosti mwaka huu
kutwaa ubingwa wa dunia wa WBF baada ya kumpiga Phil Williams wa
Marekani kwa pointi, Dar es Salaam.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment