Tuesday, 24 September 2013

WASIMULIA MKASA MZIMA WA UTEKAJI WESTGATE SHOPPINGA MALL...

  

Jengo la Wesgate Shopping Mall mjini Nairobi.
Manusura katika shambulizi la kigaidi katika duka kubwa la Westgate jijini Nairobi, Kenya, wamesimulia mkasa mzima na kusema walivyoshuhudia wateja wenzao katika duka hilo wakiuawa baada ya kubainika kutokuwa Waislamu.

Wateja hao walisema walipangwa mstarini na kuuawa baada ya kushindwa kukariri mistari ya Korani na hadi jana watu 62 walikuwa wameuawa, wakiwamo Waingereza watatu, katika mashambulizi ambayo kikundi cha kigaidi cha al Shabaab chenye uhusiano na al Qaeda, kinadai kuhusika.
Baadhi ya wateja walijificha ndani ya stoo za duka hilo, huku wengine wakiingia kwenye makasha tupu ya bidhaa au kujifanya wamekufa.
Wengi walikuwa wakikimbia mauaji hayo yaliyokuwa yakiwanyemelea baada ya kushuhudia wateja wenzao wakiuawa bila huruma baada ya kubainika kutokuwa Waislamu.
Wanaume, wanawake na watoto walikuwa wakipangwa na kuuawa kwa bunduki aina ya AK-47 baada ya kushindwa kutaja jina la mama wa Mtume Muhammad au kukariri mistari ya Korani, hivyo kuitwa makafir au wasio na imani.
Wengine walikimbia na kujificha ndani ya maduka, benki na stoo wakati mabomu ya kurushwa kwa mkono yakilipuliwa na risasi zikiwakosakosa.
Waliobahatika kunusurika walijitokeza wakiwa wametapakaa damu huku wamejawa hofu, na majeruhi wakiondolewa nje wakisukumwa kwenye vitoroli vya kununulia bidhaa dukani humo.
Mmoja wa manusura hao,  Hannah Chisholm (21) kutoka Haslemere, Surrey, alielezea hali ya kutisha na kuchanganya iliyokuwa katika duka hilo, ambalo aliamua kulitembelea kama sehemu yake ya likizo.  
Alisema: “Tulikuwa tunakimbia huku na huko lakini risasi zilikuwa zikiendelea kurindima hivyo tukaamua kujificha katika chumba cha stoo, idadi yetu tukiwa zaidi ya 60.
“Miongoni mwetu walikuwamo watoto na mtu mwingine aliyekuwa amepigwa risasi. Awali tulidhani watu hao wenye silaha walikuwa ni wezi, hivyo tuliamini kwamba wasingeweza kufika mahali tulipokuwa.” 
Greg Aldous kutoka New Zealand, alisimulia jinsi alivyojificha kwenye kasha na kuona mtu akipigwa risasi umbali wa futi 30 kutoka alipokuwa. Alisema magaidi hao “walikuwa wanaingia kutoka mlango wa mbele na wa nyuma nasi tulikaa kimya.”
Aliongeza: “Hawa ni Waislamu wenye msimamo mkali. Walikuwa wakiua mtu yeyote. Wanatisha.”  Baadaye aliweza kutoroka kutokana na kiza hadi eneo la maegesho ya malori ya mizigo ambako alikuta wengine wamejawa na hofu na wengine wakilia.
“Hisia zangu zilikuwa zinanituma nijifiche, niliingia ndani ya kasha kubwa lililokuwa na katoni za bidhaa za duka hilo na kujificha humo,” alisema. “Nilinusurika mauaji hayo kwa sababu niliondoka eneo la shambulio. Mtangazaji wa redio, Saadia Ahmed ni mmoja wa watu 1,000 waliokimbia. Alisema: “Nilishuhudia watu wachache wakiinuka na kuzungumza Kiarabu na kisha magaidi hao kuwaachia. Rafiki yangu alijitambulisha kuwa Mwislamu na kutamka neno kwa Kiarabu naye akaachiwa. Kama wangeniona …mimi ni Mzungu, ningekufa. Wasingefikiria mara mbili. Wanachukia rangi yako.”
Lakini akaongeza: “Niliona watoto wengi na wazee wakiuawa. Sielewi ni kwa nini uue mtoto wa miaka mitano! Walikuwa wakifyatua ovyo risasi kwa mtu yeyote aliyejaribu kutoroka.”
Mama mmoja, Kamal Kaur, ambaye alikuwa akinunua bidhaa akiwa na familia yake, alituma ujumbe wa kushitua kwa Twitter  kuhusu tukio hilo alipofika nyumbani: “Nilishika nywele zangu na kulia kwa huzuni kama mtoto. Damu ilitapakaa kichwani. Haikuwa yangu. Yule mtoto mdogo aliyekufa karibu yangu … Mwanangu wa kiume alinusurika kufumuliwa kichwa. Risasi ilimkosa kwa inchi moja. Iligonga ukutani. Iliporudi ilimpata mtoto mdogo wa kiume aliyekuwa jirani yake ikamuua”.
Mhandisi wa Mawasiliano ya Teknolojia, Charles Karani (41), alisema: “Nilijificha chini ya gari na binti zangu, na niliona watu hao wakipanga watu wapatao 40 na kuuliza waliokuwa Waislamu, na kama walikuwapo, ili kuthibitisha waliwataka kutamka jina la mama wa Mtume Muhammad. Waliokosea walipigwa risasi. Damu ilitapakaa kila mahali.
“Wanawake wawili waliokuwa chini ya gari na mimi walikuwa na majeraha ya risasi miguuni. Wengine kwa uhakika walikuwa tayari wamekufa. Niliona wanne wamelala, hawatikisiki.  Bomu la kutupa kwa mkono lilirushwa na kuviringika hadi tulipokuwa. Binti yangu akasema: ‘Baba, bomu hilo’-lakini tunashukuru Mungu halikulipuka na nikalipiga teke likasogea mbali.”
Mwanamke mmoja, aliandika kwenye Twitter kwa jina la Shirley Ghetto, akisimulia jinsi alivyojificha chini ya magodoro dukani humo. Aliandika akiwasiliana na watu: “ Je, ni salama kujitokeza? Kuna ukimya. Tafadhali naomba unijulishe hali ilivyo.”
Ofisa wa Umoja wa Afrika (AU), Fred Ngoga Gateretse, alitambaa sakafuni na kuona magaidi hao wakifyatulia risasi wateja na polisi. “Niaminini, watu hawa ni wadunguaji,” alisema.
“Ni dhahiri kuwa wana mafunzo maalumu.”
Vikosi vya Kenya vilionekana vikiwa na makombora wakati vikiingia katika duka hilo juzi baada ya helikopta za Jeshi kupita juu ya duka hilo.
Awali maofisa wa usalama hawakusema idadi ya watu waliokuwa wanashikiliwa mateka. Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya kilisema, kikikariri Polisi, kwamba watu 49 ndio walioripotiwa kupotea.
Idadi hiyo bila shaka ndiyo iliyotumiwa kama ya watu waliokuwa wanashikiliwa na magaidi hao. Wasio Waislamu ndio hasa walikuwa walengwa wa shambulio hilo.
Msalaba Mwekundu juzi usiku uliongeza kuwa idadi ya vifo iliongezeka kutoka 59 hadi 68 baada ya miili tisa zaidi kupatikana katika operesheni hiyo ya uokoaji, lakini hata hivyo jana Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph ole  Lenku alisema idadi ya waliopoteza maisha ni 62.
Awali ilisemekana kuwa magaidi hao miongoni mwao walikuwa wanawake, ingawa Lenku alisema wote walikuwa wanaume na baadhi yao walivalia kike.
Waasi wa Kiislamu walisema shambulizi hilo lilikuwa ni la kulipiza kisasi kwa hatua ya Kenya kupeleka vikosi vyake Somalia mwaka 2011 kupambana nao.
Msemaji wa al Shabaab alisema kupitia televisheni, kwamba watu kutoka Magharibi hawatakuwa salama nchini Kenya hadi nchi hiyo iondoe vikosi vyake Somalia.
Alisema: “Wakenya wana damu viganjani mwao. Yeyote aliye tayari kuja Kenya anapaswa kujiandaa kukabiliana na hali halisi.
“Hatuogopi watu kutoka Ulaya na Marekani kwa sababu sisi si dhaifu. Na tunawaambia hao Wazungu, kwamba yeyote ambaye amekuwa akisaidia waliokuwa wakitushambulia, waambieni Wakenya kuacha mashambulizi yao kama wanataka kubaki salama.”
Al Shabaab ilisema kupitia mtandao wao mpya wa Twitter- baada ya ule wa awali kufungwa Jumamosi-kwamba maofisa wa Serikali ya Kenya walikuwa wanawataka watekaji kuzungumza nao.
“Hatutazungumza na Serikali ya Kenya ilhali vikosi vyake vinavamia nchi yetu, hivyo kuleni matunda machungu kutoka kwenye mavuno yenu,” al Shabaab iliandika.
“ Kwa muda mrefu tumepigana vita na Kenya ndani ya ardhi yetu, sasa ni wakati wa kuhamishia vita ndani ya ardhi yao.”
Iliongeza: “Wakenya hawatajua uzito wa tatizo bila kuona, kuhisi na kushuhudia vifo kwa sura zote.”
Duka hilo ambalo ni maarufu na linatumiwa na Wakenya matajiri na wataalamu wa kigeni, lilitapakaa miili ya watu katika madimbwi ya damu. Baadhi yao waliuawa wakiwa ndani ya magari yao, huku wengine wakiondoka na majeraha makubwa.
Wacanada wawili, akiwamo mwanadiplomasia Annemarie Desloges, na wanawake wawili wa Kifaransa walithibitika kuwa miongoni mwa waliouawa, sambamba na mshairi maarufu wa Ghana Kofi Awoonor.  Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani nayo ilisema raia wanne wa nchi hiyo ni miongoni mwa waliojeruhiwa.
Mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya binafsi, Jonathan Maungo aliiambia Reuters: “Waliingia kupitia damu na ndivyo pia watakavyoondoka.”
Mtangazaji wa BBC, Anne Soy akizungumzia duka hilo alisema: “Hili ni duka kubwa – ni moja ya maduka ya aina yake jijini Nairobi. Mara zote huvutia wageni na Wakenya matajiri, wengi wakiwa ni wenye asili ya India. Hali ambayo ni mtambuka kwa rangi, kabila na uraia.”
Wateja wenye hofu walisimulia jinsi walivyojificha na kuomba wasionwe na wanamgambo hao. Na pale njia ilipoonekana kuwa wazi akina mama waliokuwa wakilia, walipakata watoto wao wadogo na kutoka nje ya duka hilo la ghorofa nne na wanaume waliotapakaa damu. 
Katika mgahawa, mwanamke na mwanaume walionekana wamelala chini wamekufa huku wamekumbatiana, kabla miili yao haijaondolewa huku muziki katika mgahawa huo ukiendelea kusikika kwenye redio. 
Nahashon Mwangi alikuwa kazini alipopokea simu kutoka kwa mwanawe wa kiume, akimwomba amwokoe kutokana na kifo ambacho kilikuwa kinamjongelea.
“Baba, nimepigwa risasi shingoni na mkononi. Navuja damu sana. Njoo unisaidie tafadhali,” mwanawe huyo wa miaka 21 alisema.
“Ilinichukua kama saa moja hivi kufika eneo hilo,” Mwangi alisema. “Nilikuwa nalia nikiomba polisi wamwokoe mwanangu. Nakumbuka  kulia kama mtoto, nililia na kulia lakini hawakuniruhusu kuingia.”
Faraja ilimjia saa tano baadaye, pale mwanawe huyo aliyejeruhiwa alionekana miongoni mwa watu waliopatikana na kuokolewa na vikosi vya usalama vilivyokuwa vikipita duka baada ya duka. Alikimbizwa katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan na kufanyiwa upasuaji.
“Naomba apone,” baba huyo mwenye mshituko alisema. “Kwa nini watu hawa watufanyie hivi?” alihoji.  Mwathirika mwingine, mfanyakazi wa duka hilo, Zipporah Wanjiru, akitoka kwenye kadhia hiyo akiwa hai lakini mwenye mshituko alisema:
“Walikuwa wakizungumza lugha fulani hivi ambayo sikuwa naielewa, sikuelewa chochote – lakini sauti zao zilikuwa kali.”
Jana asubuhi al Shabaab ilituma ujumbe mwingine ukisema: “Saa 14 za mapambano zimetumia risasi 1,400 na maisha ya watu 140 yatapotea kwa kulipiza kisasi. Asubuhi njema Kenya!”
Uliongeza kuwa walikuwa bado ndani ya duka hilo, wakipigana na makafir wa Kenya ndani ya uwanja wao na kutangaza: “Haki inapokataliwa, itadaiwa kwa nguvu. Wakenya walikuwa salama katika majiji yao kabla ya kutuvamia na kuua Waislamu.”
Kikundi hicho cha magaidi kilidai kimeshaua zaidi ya Wakenya 100 makafir.  Msimamizi wa mochwari ya Nairobi, Sammy Nyongeza Jacob alisema miili ya Waafrika, Waasia na wenye damu mchanganyiko wa Waasia na Wazungu ni miongoni mwa iliyofikishwa hapo baada ya shambulizi hilo.

0 comments:

Post a Comment