Tuesday, 1 October 2013

MKENYA 'ALIYEMTEKA' DK ULIMBOKA ATOZWA FAINI SHILINGI 1,000...


  

Dk Steven Ulimboka akiwa hospitalini mara baada ya kushambuliwa.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh 1,000, raia wa Kenya, Joshua Muhindi baada ya kupatikana na hatia ya kutoa taarifa za uongo kwa Ofisa wa Polisi.

Hukumu hiyo ilitolewa mahakamani hapo jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Aloyce Katemana.
Muhindi alinusurika kwenda jela baada ya kulipiwa faini hiyo ya Sh 1,000 na mwandishi wa habari wa Times FM, Chipangula Nandule.
Awali kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Muhindi alitakiwa kujitetea, ambapo  alidai kuwa alilazimika kutoa taarifa za uongo kutokana na alichosema ni kulazimishwa kufanya hivyo na watu asiowajua, kwa madai kuwa walimtishia maisha.
Alidai kuwa alitekwa na mtu asiyemfahamu akiwa na silaha na kumpeleka   Dar es Salaam na kumtaka kufuata maelekezo na ndipo mtu huyo alipomtaka kutoa taarifa hizo ambapo alizitoa katika Kanisa la Ufufuo na Uzima maeneo ya Tanganyika Packers, Kawe.
Aliiomba Mahakama kumpa adhabu itakayokuwa funzo kwa watu wengine lakini pia kuzingatia kuwa bado ni kijana na anategemewa na mama yake ambaye ni mjane.
"Siwezi kuilaumu Serikali, upande wa mashitaka ama Polisi, najilaumu mwenyewe kwa kutoa taarifa hizi. Taarifa hizi nilizitoa Polisi kwa hiari yangu wala sikutishwa, lakini nilifanya hivyo kwa kuhofia usalama wangu kutokana na vitisho nilivyopewa awali, na hasa kwa kuwa Tanzania si nchini kwangu," alidai Muhindi.
Hata hivyo, baada ya utetezi wake huo, Hakimu Katemana alisema Mahakama imemtia hatiani kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na baada ya kukiri kuwa alitoa taarifa za uongo kwa Ofisa wa Polisi.
"Baada ya kuzingatia kosa lililokutia hatiani, pia kukaa gerezani muda mrefu na yale uliyoomba, Mahakama inakuamuru kulipa faini ya Sh 1,000 au kwenda jela ikiwa utashindwa kulipa faini hiyo," alisema Hakimu Katemana.
Adhabu hiyo ilitolewa kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 122 vifungu vidogo (a) na (b)  ambavyo kwa pamoja vinasema mtu yeyote atakayetoa taarifa za uongo kwa Ofisa wa Serikali na akapatikana na hatia, adhabu yake itakuwa ni kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh 1,000 au kutumikia vyote kwa pamoja.
Awali akimsomea maelezo ya awali kabla ya hukumu, Wakili wa Serikali Tumaini Kweka alidai kuwa mshitakiwa akiwa raia wa Kenya eneo la Murang'a, aliingia nchini kupitia mpaka wa Namanga na kufika Dar es Salaam.
Aliendelea kudai kuwa Julai 29, mwaka jana akiwa mmoja wa waumini waliohudhuria ibada katika Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Gamanywa, alifanya maungamo mbele ya Mchungaji Joseph Kiriba akidai kuwa yeye ni mmoja wa watu waliohusika kumteka na kumtesa na baadaye kumtupa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Steven Ulimboka.
Alidai kuwa Julai 7  mwaka jana askari walimkamata na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, kwa mahojiano ambapo alikiri kuhusika na tukio hilo.
Wakili Kweka alidai Julai 13 mwaka huu, Muhindi alipelekwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Kawe mbele ya Hakimu Mlinzi wa Amani ambapo alikanusha maelezo aliyotoa awali Polisi.
Awali Muhindi alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kesi ya kumteka na kujaribu kumwua Dk Ulimboka.
Hata hivyo, baada ya upelelezi kufanyika ilibainika kuwa hakuhusika hivyo kufunguliwa mashitaka ya kutoa taarifa za uongo kwa Ofisa wa Jeshi la Polisi.
Ilidaiwa katika mashitaka mapya kuwa Julai 3 mwaka jana, katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, Muhindi alitoa taarifa za uongo, kuwa yeye na wenzake wasiojulikana, walikodishwa kumteka na kumwua Dk Ulimboka jambo ambalo si kweli. Muhindi kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo Julai, mwaka jana.

0 comments:

Post a Comment