Walinzi wakikagua moja ya magari mjini humo. |
Vichwa sita vilivyochinjwa vya
binadamu vimepatikana kwa zaidi ya siku mbili katika mji mmoja nchini
Mexico ambako wakazi wa mjini humo wameunda vikosi vya kujilinda dhidi
ya magenge ya matajiri wa dawa za kulevya.
Vichwa hivyo vilivyopatikana Ijumaa vilitelekezwa kwenye sanamu mjini Los Reyes, Msemaji wa maendesha mashitaka wa jimbo la Michoacan, Alejandro Arellano alisema.
Vichwa hivyo vyote vilikuwa vya wanaume na vilikuwa na majeraha ya risasi, limeripoti gazeti la The Huffington Post.
Arellano amesema kikaratasi chenye ujumbe unaotishia kundi la 'kujilinda' la mjini humo kiliachwa karibu na mabaki hayo ya binadamu.
Ujumbe mwingine uliachwa Alhamisi - lakini mamlaka zilikataa kuweka bayana kilichoandikwa ndani yake.
Makundi ya 'kujilinda' mjini Los Reyes yamekuwa yakipambana na wasafirishaji wa dawa za kulevya katika miezi ya hivi karibuni.
Makundi haya yamekuwa yakiundwa katika jimbo la Michoacan. Wanasema wanapambana na utekaji nyara, mauaji na vitendo vingine vya uhalifu ambavyo magenge hayo ya dawa za kulevya yanashiriki, kwa mujibu wa gazeti la The Latin Times.
Mwezi uliopita, polisi waligundua miili ya wanaume wawili ikining'inia kwenye mti katika mji huo wa Los Reyes sambamba na ujumbe unaotishia vikundi vya 'kujilinda' katika jamii hiyo.
Mexico imeshuhudia wimbi la uhalifu unaohusiana na genge la dawa za kulevya hivi karibuni. The Huffington Post limeripoti kwamba wanaume wawili waliojifunika sura zao walimimina risasi ndani ya baa huko Nueva Leon Alhamisi, na kuua watu wanne na kujeruhi wengine wawili.
Wahalifu hao waliripotiwa kuwasili wakiwa ndani ya taksi katika baa hiyo huko Santa Caratina, kitongoji kimoja cha jiji la Monterrey, wakaingia ndani na kumimina risasi na kisha kutoweka kwa kutumia taksi hiyo hiyo.
Nuevo Leon imeshuhudia wimbi la uhalifu uliosababishwa na mapigano kati ya Zetas na genge la dawa za kulevya la Gulf tangu vikosi vya zamani vya ushirika viliposambaratika mwaka 2010.
0 comments:
Post a Comment