Tuesday, 16 July 2013

WINGU LATANDA WANAJESHI WA TANZANIA DRC


WINGU zito limetanda kwa askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), katika nchi za Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Wakati Watanzania wakiendelea kuomboleza vifo vya wanajeshi saba wa jeshi hilo waliopoteza maisha katika Jimbo la Darfur, Sudani kwa kushambuliwa na waasi, nchini DRC yamezuka mapigano makali baina ya waasi na majeshi ya Serikali.

Mapigano hayo yameripotiwa kuibuka kati ya Wanajeshi wa Serikali na waasi karibu na mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Msemaji wa wapiganaji wa waasi wa M23, ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa ndege za kivita za Serikali zimefanya mashambulio ya anga katika maeneo yao usiku wa kuamkia jana.

Umoja wa mataifa kwa upande wake umesema uko tayari kutumia nguvu, kuwalinda raia ikiwa wapiganaji hao wa M23 wataingia katika mji wa Goma.

Raia wakimbia mapigano

Wakati huo huo, mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu, yamesema kuwa zaidi ya wakimbizi elfu sabini raia wa Congo wamekimbilia nchi jirani ya Uganda, kukwepa mapigano hayo.

Wapiganaji wa waasi wa Uganda nchini Congo, Allied Democratic Forces walishambulia mji wa Kamango na kusababisha mapigano makali kati yao na jeshi la serikali.

0 comments:

Post a Comment