Waziri Mkuu Mizengo Pinda. |
Watanzania wametakiwa kuelekeza
nguvu zao kusaidia vijana wanaojiajiri kwa kuwawezesha kupata huduma
muhimu za chakula na miundombinu muhimu ya maji na umeme.
Mwito huo ulitolewa jana mjini hapa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akitoa hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge.
Waziri Mkuu alizitaka wizara na taasisi zenye dhamana na kilimo, kusaidia vijana hao kupata pembejeo na zana bora za uzalishaji mali ili miradi yao iweze kuongeza uzalishaji na hatimaye kufikia kiwango cha kujitegemea.
Akisisitiza viongozi wa halmashauri kuwajibika ipasavyo na kutumia fedha za umma kwa manufaa ya Taifa, huku viongozi wahusika na ushirika wakisaidia na kuongoza vijana waliojiunga kujisajili kisheria ili wakopesheke.
Uongozi wa wilaya na mikoa ulitakiwa nao kushirikisha vikundi vyote vya taasisi vikiwamo vyama vya siasa, madhehebu ya dini na watendaji wengine kusaidia vijana hao na kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo yenye miradi yao, wananufaika na ujuzi wao na hatimaye kubadilisha maisha yao kwa ujumla.
Kwa upande wa viongozi wa mikoa na halmashauri, Waziri Mkuu aliwataka kutambua kuwa vijana hao bado wanahitaji kulelewa kimaadili, hivyo wawe karibu nao kwa kuwapa semina za malezi ikiwamo michezo na burudani.
“Vyuo vingine vya elimu ya juu viweke mipango madhubuti ya kusaidia wahitimu wa fani zilizo katika vyuo hivyo kuanza ushirika,” alishauri Waziri Mkuu ambaye alieleza kuvutiwa na vikundi vya vijana.
Akifafanua, alivitaja vikundi hivyo kuwa ni pamoja na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUGECO) ambao wanaendesha takriban miradi ya kilimo 11 ukiwamo ufugaji samaki, kuku, nguruwe na nyuki, kukausha mboga na matunda na kukamua mafuta ya alizeti.
Kingine ni kikundi cha vijana wapatao 86 wa “Pathfinders Green City” katika vijiji vya Tumbili na Lufwisi wilayani Sikonge, Tabora; cha Graduates Integrated Youth Association (GIYA) cha Igunga ambacho kimepewa ekari 300 na wilaya kwa ajili ya kilimo cha alizeti na vitunguu.
Waziri Mkuu alieleza pia kuvutiwa na mfumo wa maisha ya vijana ya kuishi katika makambi, kwa mfumo wa Maisha Plus.
Kuhusu dawa za kulevya, Waziri Mkuu alisema tukio la Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) Julai 5 ambapo watu walikamatwa nazo, baada ya taarifa hizo kupatikana, kamati ndogo ya ulinzi na usalama ya uwanja huo ilikutana Julai 9 na kuagiza uchunguzi uanze mara moja.
"Kwa utaratibu, jalada lilifunguliwa, watuhumiwa kuhojiwa na hatimaye jalada hilo kupelekwa kwa Mwanasheria wa Kanda ya Dar es Salaam Julai 29, kwa ajili ya uamuzi wa kisheria. Taratibu za kukamilisha uchunguzi wa tukio hili zinaendelea," alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alikiri kwamba vita dhidi ya dawa hizo haiwezi kukomeshwa na nchi moja, kwa hiyo mapambano dhidi ya wafanyabiashara wa dawa hizo yatafanikiwa kwa nchi zote duniani kuungana katika kudhibiti biashara hiyo.
Akizungumzia ujio wa viongozi wakubwa duniani, alisema kimsingi, ujio wa viongozi hao mashuhuri katika kipindi kifupi, pamoja na wengine wengi kutoka nchi za Afrika na sehemu zingine ni uthibitisho thabiti wa kuimarika kwa demokrasia ya ndani, amani na utulivu, utawala bora na mazingira bora ya uwekezaji.
"Kwa ujumla mafanikio yanayotarajiwa kupatikana kutokana na ujio wa viongozi ni mengi, lakini ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania na nchi zingine, kufaidika na mitaji ya maendeleo kwa ajili ya kujenga miundombinu; na kufunguka milango ya uwekezaji.
"Ziara za viongozi hao zimetoa fursa kwa wawekezaji kote duniani kuona mazingira mazuri na fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini," alisema Pinda.
Kuhusu bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, Waziri Mkuu alisema hadi sasa meli nne kati ya 12 zimewasili nchini zikiwa na shehena ya vipande 16,623 vya mabomba ambayo yameanza kusambazwa katika maeneo husika.
Mabomba hayo yatawezesha ujenzi wa bomba wa umbali wa kilometa 194 kati ya 532 za umbali wa mradi wote. Kazi ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa mradi inaendelea, mfereji wa mabomba (Mkuza) umesafishwa kwa umbali upatao kilometa 293 na kazi ya kuunga mabomba ilianza Agosti 26.
Alisema kazi ya kulaza bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam inatarajiwa kukamilika Juni mwakani na kukamilika kwa mradi wote Desemba.
Aliwataka wapinzani ambao waliamua kususia mjadala wa Muswada wa sheria ya Marekebisho ya Katiba, kujirudi na kutumia busara hatimaye kurudi kushiriki mchakato wa Katiba mpya.
Pamoja na masuala mbalimbali ya maendeleo na mafanikio aliyoyabainisha katika hotuba yake, Waziri Mkuu aliahirisha Bunge hadi Oktoba 29.
0 comments:
Post a Comment