Askari wa Kikosi Maalumu cha Anga (SAS) cha Uingereza, ameonekana shujaa
katika tukio la uvamizi lililotokea katika jengo la maduka la Westgate
jijini Nairobi Kenya baada ya kufanikiwa kuokoa watu 100 waliokuwa ndani
ya jengo hilo.
Askari huyo ambaye jina lake halikutajwa kutokana na kile kilichoelezwa
kuwa ni sababu za kiusalama, wakati wavamizi hao wanavamia jengo hilo
siku ya Jumamosi, naye alikuwemo ndani ya jengo hilo akinywa kahawa.
Kwenye baadhi ya mitandao, askari huyo ameonekana akiwasaidia wanawake
wawili huku akiwa ameweka bastola kwenye suruali yake, ingawa sura yake
imefichwa.
Habari zinasema kuwa, askari huyo ameonekana shujaa kwani licha ya hali
tete iliyokuwa ndani ya jengo hilo, aliweza kuingia na kutoka zaidi ya
mara 12 akiwaokoa baadhi ya watu waliokwama ndani ya jengo hilo lenye
maduka na migahawa mbalimbali.
“Alichofanya ni kitendo cha kishujaa sana, alikuwa akinywa kahawa na baadhi ya rafiki zake wakati wavamizi walivyoingia.
Alirudi ndani mara 12 na kufanikiwa kuokoa zaidi ya watu 100. Fikiria
kuthubutu kurudi ndani huku akijua kabisa jinsi hali ilivyo ndani ya
hilo jengo,” baadhi ya mashuhuda walinukuliwa.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, askari huyo wa Uingereza anafanya zaidi
shughuli zake Kenya na nje ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia
raia wa nchi yake wanaojishughulisha na mambo mbalimbali.
Agosti mwaka huu, gazeti la Daily Mirror liliripoti kuwa kikosi maalumu
cha SAS na askari maalumu wa kupambana na ugaidi, wameanza kumtafuta
Samantha Lewthwaite, Mwanamke anayetajwa kuwa ni raia wa Uingereza
anayedaiwa kuwa gaidi ambaye pia anashirikiana na kundi la Al-Shabaab.
Mwanamke huyu mjane anayetajwa kuwa ni gaidi, inasemekana pia alishiriki kupanga na kutekeleza uvamizi mjini Nairobi.
Kikosi hicho cha SAS, kinaelezwa kuwa kinafanya kazi kwa ukaribu na
vikosi vya ulinzi vya Uingereza, Kenya na vile vya nchi nyingine za
Afrika Mashariki.
Habari juu ya askari huyo zimekuja wakati milio ya risasi ikizidi
kusikika ndani ya jengo hilo, huku maofisa wa usalama wa nchi hiyo
wakisema kuwa wamedhibiti sehemu kubwa ya jengo hilo. Habari zaidi
zinasema kuwa, bado zaidi ya watu 10 wanashikiliwa ndani ya jengo hilo
kama mateka.
‘Tumeshadhibiti sehemu yote ya jengo, tuko hapa kuhakikisha tunawaadhibu
vya kutosha hawa watekaji,” Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Kenya, IGP David
Kimaiyo aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter.
Licha ya maelezo hayo, mpaka jana saa 12 asubuhi bado milio ya risasi ilikuwa ikizidi kusikika ndani ya jengo hilo.
Kundi la Al-Shabaab, lililodai kuhusika na tukio hilo, juzi liliweka
ujumbe wa sauti kwenye baadhi ya mitandao likidai kuendelea kushikilia
sehemu kubwa ya jengo hilo. “Licha ya juhudi zinazofanywa, bado
tunaendelea kushika sehemu ya jengo la Westgate,” Msemaji wa Al-Shabaab
Sheik Ali Mohamud anasema.
Mtandao wa Daily Mail unasema kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya,
Amina Mohamed anasema raia watatu wa Marekani na mmoja wa Uingereza, ni
kati ya watu waliovamia jengo hilo la Westgate.
“Mvamizi kutoka Uingereza ni mwanamke ambaye amekuwa akijaribu
kutekeleza uvamizi kama huu mara nyingi,” anasema Mohamed akimlenga
Samantha Lewthwaite, anayedaiwa kuwa gaidi wa kimataifa.
Marekani imesema kuwa, inaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kama
kuna raia wake yeyote aliyehusika kwenye tukio hilo ambalo mpaka sasa
limegharimu maisha ya watu zaidi ya 60.
Makala haya yameandikwa na Fredy Azzah kwa msaada wa vyombo vya habari.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment